
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali ukiukwaji wa “wazi na usio na msingi” wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na Marekani katika Lango Bahari la Hormuz.
Katika taarifa, Wizara hiyo imeonya kuwa kitendo chochote cha uchokozi hakitaachwa bila majibu stahiki.
Aidha taarifa hiyo imebaini kuwa: “Kufanyika kwa vitendo hivi vya kichokozi, wakati huu ambapo mchakato wa kidiplomasia unaosimamiwa na Pakistan ukiendelea, kumebainisha tena nia ovu na ukosefu wa uaminifu wa utawala wa Marekani mbele ya taifa la Iran, watu wa eneo hili, na jumuiya ya kimataifa”.
Ingawa taarifa hiyo haikufafanua kwa kina aina ya ukiukwaji huo, mashirika ya habari nchini Iran yaliripoti kusikika kwa milipuko nyakati za usiku Jumatatu katika maeneo ya pwani ya mashariki mwa Bandar Abbas, karibu na Sirik na Jask.
Kwa upande mwingine, msemaji wa kamandi ya jeshi la Marekani, CENTCOM, Timothy Hawkins, alikiri kuwa vikosi vya Marekani vilitekeleza mashambulizi kusini mwa Iran siku ya Jumatatu, akidai kuwa yalikuwa “mashambulizi ya kujihami” yaliyolenga maeneo ya kurushia makombora na boti za jeshi la Iran zilizodaiwa kujaribu kutega mabomu ya majini karibu na mji wa kimkakati wa Bandar Abbas.
Hata hivyo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza siku ya Jumanne kuwa vitengo vyake vya ulinzi wa anga vimefanikiwa kuitungua ndege ya kivita ya Marekani isiyo na rubani au droni aina ya MQ-9 Reaper katika anga ya Ghuba ya Uajemi. Aidha IRGC imesema katika operesheni hiyo imelazimisha kurudi nyuma ndege ya ujasusi ya Marekani aina RQ-4 Global Hawk pamoja na ndege ya kivita ya F-35.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza msimamo thabiti wa Iran katika nyanja zote tatu: uwanja wa vita, mitaani, na diplomasia. Ilieleza kuwa msimamo huo unatokana na “shaka kubwa dhidi ya utawala wa Marekani ambao asili yake ni uovu na jinai dhidi ya watu wa Iran.”
Mashambulizi haya mapya ya Marekani yanakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopatikana kwa upatanishi wa Pakistan, ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yamesitisha vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran tangu mapema mwezi Aprili.
