
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu nchini Lebanon, Hizbullah, imetangaza kutekeleza mfululizo wa operesheni 32 za kijeshi dhidi ya majesh vamizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yanayofanya chokochoko kusini mwa nchi hiyo.
Katika taarifa, Harakati hiyo ya Mapambano imeeleza kuwa, wapiganaji wake shujaa wamekabiliana na jaribio la majeshi ya Israel kusonga mbele kupitia mapambano ya ana kwa ana katika nchi kavu. Mapambano hayo yaliambatana na mashambulizi makali ya makombora, mizinga, na droni, yakilenga zaidi maeneo ya mji wa kimkakati wa Zawtar al-Sharqiya. Operesheni hizo 32 zimetekelezwa katika kipindi cha amsaa 24 kufikia Jumanne jioni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Hizbullah, operesheni hizo zimefanikiwa kuharibu na kuharibu kabisa vifaru kadhaa vya Merkava pamoja na magari ya deraya ya utawala huo ghasibu. Aidha, wapiganaji hao wamelemaza mifumo ya mawasiliano, kupiga moja kwa moja mtambo wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome, na kudungua droni mbili ndogo (quadcopters) za kijasusi za utawala huo.
Mashambulizi haya yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa na uthabiti, yanadhihirisha azma ya Hizbullah ya kulinda mamlaka ya ardhi ya Lebanon na kuwahifadhi wananchi wake dhidi ya ukiukwaji wa mara kwa mara na uvamizi wa kichokozi wa utawala wa Tel Aviv.
Harakati hiyo ya Mapambano ya Kiislamu imethibitisha kwa mara nyingine kuwa jeshi la uvamizi la Kizayuni haliwezi kukanyaga ardhi ya Lebanon bila kulipa gharama kubwa. Hizbullah imesisitiza kuwa operesheni zake ni za kujihami kwa lengo la kumlazimisha adui kuondoa majeshi yake yote kusini mwa Lebanon na kukomesha jinai na uchokozi wa utawala huo haramu.
Hali hii inakuja huku kukiwa na ripoti za kusikitisha ambapo mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni yamesababisha vifo vya kishahidi vya zaidi ya watu 3,100 nchini Lebanon tangu uvamizi huo uongezeke kuanzia tarehe 2 Machi.
