Wapalestina wa Gaza katika jinamizi badala ya sherehe wakati wa Eid el-AdhaWapalestina wa Gaza katika jinamizi badala ya sherehe wakati wa Eid el-Adha

Ikiwa leo ni sikukuu ya Eid El-Adha, Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel hawana cha kusherehekea bali wanakumbwa na jinamizi na masaibu yaliyosababishwa na utawala huo ghasibu.

Badala ya kusherehekea sikukuu hii, watoto wa Gaza wanajihusisha na uchuuzi wa bidhaa ndogo ndogo ili waweze kukimu familia zao.

Eid ul Adha, inawadia huku Ukanda wa Gaza ukiendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita na kuporomoka kwa uchumi baada ya vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa Israel dhidi ya eneo hilo Oktoba 2023. 

Tangu wakati huo Wapalestina wasiopungua 73,000 wameuawa shahidi wengi wakiwa ni wanawake na watoto huku karibu makazi yote ya eneo hilo yakiwa yameharibiwa.

Aidha wakati Waislamu kutoka pembe zote za dunia wameifika Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ambayo ni miongoni mwa nguzo za Uislamu, wengi wa Wapalestina wa Gaza wanasalia wakiwa wamekwama kutokana na vita, mzingiro uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kufungwa kwa vituo vya mpakani na janga la kibinadamu lililotokana na vita kumewanyima maelfu ya Wapalestina fursa ya kutekeleza moja ya nguzo muhimu zaidi za dini ya Uislamu.

Wakati huo huo kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watoto 637,477 wenye umri wa kwenda shule hawana fursa endelevu ya kupata elimu rasmi ya ana kwa ana. 

Watoto 64,000 wenye umri wa miaka mitano hawana fursa ya kupata elimu ya awali ya utotoni. OCHA imebainisha kuwa hali ya kibinadamu huko Gaza bado ni mbaya sana, huku familia nyingi zikiendelea kuishi katika mahema yaliyojaa watu wengi, shule, na majengo yaliyoharibiwa, katikati ya vizuizi vikubwa vya upatikanaji wa maji safi na usimamizi wa taka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *