Dili iliyokufa – 3Dili iliyokufa – 3

Jambo la ajabu lililotokea ni kuwa wakati yule dereva wa teksi anaiwasha ile teksi ili tuondoke kwenda katika hoteli nyingine ambayo hata sikujua iko wapi, fahamu zangu nazo zikazimika hapohapo. Wakati teksi inaondoka sikujijua kabisa na sina kumbukumbu ya nini kilitokea baada ya hapo.

Fahamu zilipoanza kunijia kichwani nilikuwa kama mtu ambaye bado alikuwa amelewa na aliyechanganyikiwa akili.

Kabla sijaweza kufungua macho nilihisi mwili wangu uko ovyo kama wa mtu mgonjwa na kichwa changu hakikuwa na afadhali hata kidogo. Tumbo langu lilikuwa limenichafuka na nilijihisi kama mtu aliyekuwa ametapika sana au aliyetaka kutapika.

Nikajiuliza kwanini nimepatwa na hali hiyo ambayo sikuwahi kujihisi maishani mwangu. Nikajiuliza tena, nilikuwa mgonjwa taabani? Na nilikuwa nimelala wapi?

Ubaridi niliousikia kwenye mwili wangu ndio ulionifanya nifumbue macho haraka. Nikajiona nimelala mahali kwenye kitu kigumu. Nilihisi kitu hicho kilikuwa sakafu au ubao. Na kwa kweli mahali hapo palikuwa pananiumiza.

Nilipofumbua macho sikuweza kuona kitu zaidi ya vimulimuli vilivyokuwa vinaelea hewani pamoja na mwanga ambao sikuuelewa. Macho yangu yalikuwa kama yaliyowekewa kioo kilichotiwa maji.

Lakini taratibu nikaanza kuona vizuri. Nilijiona nilikuwa nimelala ndani ya mfereji wa maji ya mvua uliokuwa kando ya barabara. Nilishituka kidogo. Nikaangaza macho yangu huku na huku nikaona polisi wawili wakiwa ndani ya mfereji huo na wawili wakiwa juu ya mfereji wakiniangalia.

Pengine polisi hao ndio walionifanya nizinduke kutoka mahali hapo nilipokuwa nimelala. Nikataka ninyanyuke kwa haraka ili nikimbie lakini mwili wangu haukukubali. Ulikuwa umechoka na kuishiwa nguvu kabisa. Zaidi ya hapo nilijihisi kama nilibebeshwa mzigo mzito kiasi kwamba isingekuwa rahisi kunyanyuka.

Kama si kuwaona hao polisi, pengine ningeendelea kulala hapohapo kwenye mfereji kwa muda usiojulikana lakini hapakulalika tena.

Wakati najitahidi kunyanyuka nikawa najiuliza, nilifikaje mahali hapo? Kabla sijapata jibu nilijiuliza tena, nilikuwa Muheza ama Dar es Salaam? Kwa kweli ndani ya akili yangu sikuwa na kumbukumbu yoyote. Nilikuwa kama zezeta.

Nikajiinua na kuketi kwenye mfereji huo huku nikijaribu kuwaza. Kwa mbali kumbukumbu zilianza kunijia. Nikakumbuka kufika Dar es Salaam. Kukutana na Dastan Lazaro aliyenipeleka katika ofisi za Shirika la Bahati Nasibu la Taifa.

Nikakumbuka nilivyozungumza na afisa mmoja wa shirika hilo ambaye aliniambia nitapewa zawadi yangu ya shilingi milioni kumi kesho yake.

Nikakumbuka nilivyopangishiwa chumba cha hoteli na nilivyorudi tena asubuhi yake katika ofisi za shirika hilo ambapo nilipewa hundi yangu ya shilingi milioni kumi.

Kufikia hapo kumbukumbu zangu zikaanza kunijia waziwazi. Nikakumbuka nilivyopewa pesa hizo benki na nilivyorudi hotelini. Nikakumbuka nilivyokwenda kwenye muziki Kinondoni, kukutana na Dastan akiwa na msichana mmoja na hatimaye msichana huyo akaniunganisha na msichana mwingine aliyeniambia ni mdogo wake.

Kumbukumbu zikaendelea kuja kichwani mwangu mpaka pale tunahama katika ile hoteli niliyofikia, nikiwa na mfuko wangu wa pesa pamoja na vitu vyangu vingine.

Kwa kweli kumbukumbu zangu ziliishia kwenye teksi. Sikuweza kukumbuka tena tulikwenda wapi na nini kilitokea. Mawazo yangu yaliishia hapohapo kama mkanda wa filamu uliofikia mwisho wake.

Kutokumbuka kilichoendelea baada ya hapo ni jambo lililonishitua sana hasa vile ambavyo nilizinduka na kujikuta nimo ndani ya mfereji huku nikiwa sijui pesa zangu na vitu nilivyonunua vimeishia wapi.

“Polisi naomba msaada wenu,” nikakurupuka kutamka maneno hayo kwa kuhisi kuwa nilikuwa nimeibiwa.

“Msaada wa nini? Hebu nyanyuka,” polisi mmoja akaniambia na kuniuliza, “Kwanini umelala kwenye mfereji?”

Kabla sijamjibu, na wala sikuwa na jibu la maana, polisi mwenzake akamjibu.

“Si unamuona huyo ni mlevi? Na ndiyo anazinduka sasa. Unafikiri pombe na bangi vina matokeo gani zaidi ya hayo?”

“Ndiyo anaonekana ni mlevi kweli. Sisi tulidhani umepigwa, kumbe ni uzembe wako. Hebu nyanyuka!”

Nikajaribu kunyanyuka kwa kushikilia kingo za mfereji. Niliona gari la polisi hao likiwa kando ya barabara. Kulikuwa kumesha kucha. Kama haikuwa saa kumi na mbili asubuhi, ulikuwa ukikaribia muda huo. Nilihisi bila shaka polisi hao walikuwa katika doria zao wakanikuta ndani ya huo mfereji.

Polisi mmoja akanipekua kwenye mifuko ya suruali yangu. Nilikumbuka nilikuwa na pesa nilizoweka mifukoni mwangu lakini wakati napekuliwa sikuwa hata na senti tano. Baya zaidi ni kwamba nilikutwa na kitu nilichofungwafungwa kwa karatasi kama pipi.

Polisi aliyekuwa akinipekua alikiangalia kisha alikinusa.

“Eh! Kete ya kokeni!” akasema na kuwaonyesha wenzake.

“Nimemkuta na kete ya kokeni. Kumbe anatumia madawa ya kulevya!”

Mwenzake akakishika kile kipipi. Naye akakinusa na kuwapa wenzake waliokuwa juu ya mfereji huku akiwaambia, “Kumbe ni teja!”

Polisi hao wakanidhibiti muda uleule.

“Twende naye!” aliyekuwa juu ya mfereji akasema.

“Lakini jamani mimi situmii kokeni,” niliwaambia polisi hao wakati wakinikokota kuelekea kwenye gari lao.

“Unasema hutumii kokeni na hiki ni kitu gani?” polisi aliyekuwa ameshika kile kipipi akaniuliza.

“Siyo changu. Nilikuwa na watu fulani jana usiku. Nafikiri wao ndiyo wameniwekea kwenye mfuko na wameiba pesa zangu.”

“Utakwenda kujieleza kituo cha polisi. Wewe tayari ni mtuhumiwa wetu.”

Nikaingizwa kwenye gari la polisi na kuwekwa katikati. Sasa tatizo lilikuwa linachukua sura nyingine. Badala ya kuibiwa pesa na vitu vyangu nilikuwa nakabiliwa na kesi ya kukutwa na kete ya kokeni ambayo sikujua ilifikaje mfukoni mwangu.

“Hii kete ya kokeni si yangu, kuna jamaa wamenitilia mfukoni,” nilitamka ghafla baada ya kuona hali inaelekea pabaya. Wakati huo gari la polisi lilikuwa linaondoka.

“Sasa wewe tumekukuta nayo, utakwenda kututajia na hao jamaa waliokupa pia tutawakamata,” polisi mmoja akaniambia.

Nilipoendelea kujitetea polisi mmoja alinitandika kibao na kuniambia ninyamaze. Kilikuwa kibao kikali kilichonipata kwenye shavu. Uchungu niliousikia ulinifanya nisisimke mwili mzima.

Nikaamua kunyamaza kimya.

Uchungu wa kile kibao, uchungu wa kuibiwa pesa zangu, na uchungu wa kubambikiwa kesi, vyote viliukaba moyo wangu ukawa unauma kama uliobandikiwa chuma cha moto.

Nikawa najiuliza aliyenifanyia ushenzi huo ni nani? Yule msichana niliyekwenda kulala naye au ni wote watatu?

Lakini kwa wote watatu isingewezekana kwa sababu nilikuwa nikimuamini sana Dastan Lazaro. Kwa vyovyote vile asingehusika na ushenzi ule.

Kwa kweli hadi leo sikumbuki eneo lile nililokutwa nimelala ndani ya mfereji ni eneo gani. Nilipopakiwa kwenye gari la polisi nilipelekwa moja kwa moja kwenye kituo cha polisi.

Nikateremshwa kwenye gari na kuingizwa ndani ya kituo hicho.

Wale polisi walionikamata wakawaambia polisi wenzao waliokuwa kwenye meza ya kaunta kuwa mimi ni mlevi wa unga.

“Tumemkuta amelala kwenye mfereji, tulipompekua tumekuta ana kete moja ya kokeni,” polisi mmoja akawaambia polisi wenzake.

“Kumbe ni teja!” polisi aliyekuwa hapo kituoni alisema na kunidaka akaniingiza ndani ya selo.

“Kete yake hii hapa,” yule polisi aliyekuwa amenipekua akaitoa ile kete.

Polisi waliokuwa kwenye kituo hicho walipoiona ilikuwa kama imewapandisha hasira kwani kila mmoja alinivutia kwake na kunitandika kibao. Polisi mmoja ndiye alinitwanga teke kabisa, vile nilivyokuwa siko sawa nilianguka chini.

“Bado amelewa, hebu amka haraka!” polisi mwingine akaniambia. Nikanyanyuka huku nikiwa nimeukinga uso wangu kwa mikono ili wasinipige.

“Simama sawa sawa,” polisi huyo akaniambia.

Nikasimama, sikuelewa kwamba alimaanisha niondoe ile mikono usoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *