Wadau kikapu waipongeza Dar CityWadau kikapu waipongeza Dar City

Dar City imetupwa nje katika robo fainali ya Kikapu Afrika (BAL) Play off, baada ya kufungwa jumla ya pointi 165-157 na Petro De Luanda ya Angola katika mechi mbili za robo fainali, huku wadau wakiipongeza na kudai ilistahili kutokana na uwekezaji iliyofanya.

Robo fainali hiyo ilifanyika katika Uwanja wa ndani wa BK Arena, Rwanda, katika mechi ya kwanza Dar City ilishinda kwa pointi 88-82, huku Petro de Luanda ikishinda ya pili kwa pointi 83-69.

Dar City ndiyo timu iliyopewa nafasi kubwa ya kutinga hatua ya nusu fainali kutokana na ushindi walioupata katika mechi ya kwanza, nafasi hiyo ingetokea endapo ingefungwa chini ya pointi sita mechi ya pili..

Mabingwa hao wa BAL 2024, iliiondoa Dar City kwa kuifunga zaidi ya pointi sita katika mechi ya pili kwa kuifunga pointi 83-69.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Shendu Hamis Mwangalla, aliipongeza Dar City kwa hatua   waliyofikia ya kucheza robo fainali.

Mwangalla aliliambia Mwanaspoti, hatua hiyo imeifanya timu hiyo kupeperusha bendera ya Tanzania katika Ligi ya kikapu ya Afrika BAL.

 “Hakika Dar City imeitangaza vyema Tanzania, imeionesha Dunia Tanzania ina uwezo mkubwa katika kikapu,” alisema Mwangalla na kupongeza uongozi wa Dar City ukiongozwa na raisi wa timu hiyo Mussa Mzenji  na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya.

“Haikuwa kazi rahisi kwani ninaelewa uwekezaji mkubwa  umefanyika ili kufika hatua hii, safari ikianzia Afrika Kusini mpaka Rwanda, pia kambi Zanzibar na Dubai,” alisema Mwangalla.

Mwangalla pia aliwaomba wadau, mashirika ya umma pamoja na mashirika binafsi yaweze kuwashika mkono katika uwekezaji wa mchezo wa kikapu.  

Raisi wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini (TBF), Phares Mageza alimpongeza naodha wa timu hiyo, Hasheem Thabeet kwa kazi kubwa aliyofanya na kuiongoza timu hiyo hadi kucheza hatua  robo fainali.

“Dar City ilionekana aina uzoefu kama timu zingine zilizoshiriki, ilikutana na timu ngumu ya Petro de Luanda ya Angola  iliyoanzishwa miaka 40 iliyopita.

Hata hivyo, aliipongeza kwa kupambana na  moja ya timu  bora Afrika.

“Timu hiyo imewahi kuwa bingwa BAL 2024, imeshinda ubingwa wa nchini mwao  mara 14, pia kuwa bingwa wa Afrika 2006, 2015,” alisema Magesa na kuongeza, Petro ina uwezo mkubwa wa kifedha,  ina uwanja wake wa ndani unaoingiza watazamaji 7000.

Dar City ilifuzu robo fainali baada ya kushika nafasi ya nne katika kundi la Kalahari Conference na timu zingine zilizofuzu katika kundi hilo ni RSSB Tigers (Rwanda), Petro de Luanda kutoka Angola) na Al Ahly Ly (Libya).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *