
Dar es Salaam. Gazeti la Mwananchi limeteuliwa kuwania tuzo ya Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) katika kundi la chomb bora cha habari nchini, zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Mwananchi imetangazwa kuwania tuzo hizo na Katibu Mtendaji wa MCT, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tuzo hizo, Ernest Sungura, leo Alhamisi, Mei 28, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kutangaza wateule wengine 12.
Wateule hao wapya wa awamu ya pili ni pamoja na waandishi wa habari sita na vyombo vya habari sita.
Tuzo ya chombo bora cha habari ni miongoni mwa vipengele vipya vya tuzo za EJAT ambazo zinatolewa kwa mara ya kwanza.
Katika orodha ya wateule wapya kundi la waandishi yumo mwandishi wa habari wa gazeti la The Citizen Julius Maricha.
Wengine ni Halima Mlacha wa Habari Leo, Hamadi Rashid wa The Loyal Media na UN Radio, Leonard Mubale wa TriGen Media, Philip Mwihava wa Clouds FM na Manyerere Jackton wa Jamhuri Media.
Wateule hao wapya wanafanya idadi ya wateule wote watakaowania tuzo hizo kufikia 24, baada ya wateule 18 waliotangazwa awamu ya kwanza, Mei 19, 2026.
Kwa upande wa vyombo vya habari mbali na Mwananchi, vingine vilivyoteuliwa kuwania tuzo hiyo ni Azam Media Group, Nukta Africa, The Guardian Newspaper, Tanzania Standard Newspapers (TSN) na Jamhuri Newspaper.
Sungura amesema kuwa tuzo ya chombo bora cha habari itatolewa kwa chombo Bora cha Habari chenye Utaalamu Maalumu wa Mwaka.
“Tuzo hii ni kwa chombo cha habari kilichoonesha ubora na kina katika sekta au eneo maalumu la habari, likichangia uelewa na mjadala wenye tija,” amesema Sungura.
Mbali na chombo bora cha habari, Sungura ametaja vipengele vingine vipya vilivyoongezeka kuwa ni Tuzo za Afya ya Uzazi za Shirika lisilo la Kiserikali linaloshighulika na masuala ya Afya Uzazi, MSI Tanzania.
Amesema tuzo hizo zinatolewa kwa wanahabari na vyombo vya habari vilivyochangia kuelimisha umma kuhusu masuala ya afya ya uzazi nchini, ikiwamo upatikanaji wa huduma, upungufu wa kisera, changamoto za vifaa tiba na athari kwa jamii.
Nyingine ni Tuzo za Uwezo Tanzania za Uandishi wa Elimu Kutambua ubora katika uandishi wa masuala ya elimu unaoangazia changamoto na ubunifu katika mfumo wa elimu Tanzania, na kutoa sauti kwa wanafunzi, walimu na wazazi.
Pia, kutakuwa na tuzo ya Chombo Bora cha Habari Kinachofuata Sheria cha Mwaka kwa chombo cha habari kilichoonesha viwango vya juu vya kufuata sheria, maadili ya uandishi na uandishi wa kitaaluma kulingana na sheria za habari Tanzania.
Vilevile kuna tuzo ya Mahojiano Bora ya Mwaka, itakayotolewa kwa mahojiano yenye matokeo chanya na makubwa, yaliyofanyika kitaaluma na kuchangia mjadala kwa umma, yakiwa yamechapishwa au kurushwa mwaka 2025.
Kipengele kingine kipya ni Tuzo ya Uhifadhi ya Mwalimu Julius Nyerere, ambayo amesema ilizinduliwa rasmi Julai 15, 2025, Arusha na Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na MCT.
Sungura amesema kuwa lengo la tuzo hiyo ni kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa ndiye aliyeweka msingi wa uhifadhi endelevu Tanzania, akiamini kuwa mazingira ni urithi wa vizazi vyote.
Sungura amesema kutokana na matumizi ya mfumo wa kiteknolojia wameweza kuandaa tuzo ya mwandishi kijana mdogo aliyefanya vizuri na mwanamke aliyefanya vizuri.
Kwa mujibu wa Sungura, tuzo hizo ambazo zitatolewa kwa washindi kesho, Ijumaa Mei 29, 2026, katika ukumbi wa Four Points by Sheraton, jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia uanzishwaji wa vipengele hivyo vipya Sungura amesema kuwa hatua hiyo inatokana na utafiti uliofanyika kwa kipindi cha mwaka jana na kuja matokeo ya ushirikishwaji na umuhimu wa EJAT.
“Mapendekezo hayo yanatokana na maoni ya waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania ambao wanaamini kuwa mfumo wa sasa hauwapi uwakilishi wa kutosha wanahabari wa kidijitali, sauti za mikoani pamoja na kazi za ushirikiano katika uandishi wa habari,” amesema Sungura.
“Utafiti huo ulijumuisha maoni kutoka kwa zaidi ya waandishi wa habari 200, wahariri, majaji, viongozi wa vyombo vya habari na wadau mbalimbali kutoka maeneo tofauti nchini.”
Mbali na vipengele hivyo ambavyo vimeanza kufanyiwa kazi, Sungura amesema utafiti huo pia ulipendekeza kuanzishwa kwa tuzo za Uandishi wa Habari za Simulizi za Mseto wa Vyombo (Multimedia Storytelling), Uchunguzi wa Habari Kupitia Mitandao ya Kijamii, Tuzo za Chaguo la Wananchi na Chombo.
Pia, Sungura amesema baraza linaona kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na ushirikiano wa kimkakati na taasisi mbalimbali ili kuimarisha ubobevu wa uandishi wa habari mahususi Tanzania.
“Ushirikiano wa aina hii umeonesha kuwa na mafanikio katika uandishi wa habari kwa sababu unawatengeneza waandishi wa habari waliobobea kwenye eneo fulani, kitu ambacho hapa nchini hakipewi kipaumbele,” amesema Sungura.
Mkurugensi MSI (awali marie Stopes) Patrick Kinemo amesema wamekuwa wadau wa MCT kwa muda mrefu katika kuboresha taaluma ya uandishi wa habari.
”Sisi ni wadau wakubwa wa MCT na EJAT na tunashukru kwa kutupa tuzo ambayo itatupa chachu zaidi katika kuboresha afya za Watanzania,” amesema Kinemo.
Katibu wa jopo la majaji, Mwanzo Milinga amesema vigezo 10 vilivyotumika kuwapata wateule akisema kuwa kila kigezo kina alama 10.
