Sh946 milioni zanufaisha vikundi 34 Mbeya vijijiniSh946 milioni zanufaisha vikundi 34 Mbeya vijijini

Mbeya. Zaidi ya Sh946 milioni za mikopo ya asilimia 10 zimetolewa kwa vikundi 34 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Imeelezwa kuwa awali halmashauri ilipokea maombi kutoka vikundi 55, ambapo 34 ndivyo vilivyofanikiwa kunufaika na mikopo hiyo.

Hundi za mikopo hiyo zimekabidhiwa leo Alhamisi Mei 28, 2026 na Mbunge wa Mbeya Vijijini, Patali Shida, katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mabasi Tarafani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Patali amesema utoaji wa mikopo hiyo umechangia kupunguza utegemezi na vitendo vya uhalifu miongoni mwa vijana wasiokuwa na ajira.

“Tunaona namna Serikali inavyofanya kazi kubwa kuwezesha makundi haya, wakiwemo watu wenye ulemavu, kufikia hatua ya kuanzisha miradi ya kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Patali amesisitiza wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kutoa nafasi kwa makundi mengine kunufaika badala ya kuzitumia tofauti na maandiko waliowasilisha.

“Tuombe mikopo hii ilete tija kwenye miradi na kuwezesha wengine kunufaika ili kufikia dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuinua wananchi kiuchumi na kuwafanya kumudu maisha yao ya kila siku,” amesema.

Katika hatua nyingine, Patali amesema wanatambua mchango mkubwa wa maofisa maendeleo ya jamii, lakini bado kuna changamoto ya ukosefu wa elimu ya mikopo kwa wananchi.

“Kuna watu wanakosa mikopo kwa sababu ya kukosa elimu. Nendeni mkatoe elimu ili kutekeleza maagizo ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuona kila Mtanzania ananufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Aida Haule akizungumza na wanufaika wa mkopo wa asilimia 10 wa  zaidi ya Sh946 milioni. Picha na Hawa Mathias

Wakati huohuo, Patali amesisitiza maofisa maendeleo ya jamii kuwafikia wananchi waliokosa mikopo katika awamu hii ili kuwapa maelekezo ya namna ya kujiandaa kwa awamu nyingine.

Patali amesema mikopo hiyo imetolewa kwa uwazi huku wananchi 360 kutoka kata 18 wakinufaika. Pia, ameutaka uongozi wa halmashauri kutumia magari ya matangazo kuwafikishia wananchi taarifa za fursa za mikopo katika awamu zijazo.

Kuhusu kilio cha lumbesa

Patali amesema tayari amewasilisha hoja hiyo bungeni na kuomba kutungwa kwa sheria ya kupiga marufuku matumizi ya ujazo wa lumbesa kwenye mazao ya chakula na biashara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri, Aida Haule amesema wanaendelea kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuinua uchumi wa Watanzania kupitia mikopo ya asilimia 10.

Amesema wananchi wanashuhudia kwa uwazi namna mikopo hiyo inavyotolewa na Serikali, huku akibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka miwili zaidi ya Sh3.2 bilioni zimetolewa kwa vikundi mbalimbali.

Kauli ya CCM

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya, Hakimu Mwalupindi, amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Agness Elikunda, amesema mikopo hiyo imenufaisha vikundi 34 kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi na vikundi kiuchumi.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita halmashauri imesajili vikundi 241 vyenye sifa ya kupata mikopo, vikiwemo vikundi 111 vya wanawake, 119 vya vijana na 11 vya watu wenye ulemavu.

Aidha, amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026, halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh3.222 bilioni kwa vikundi 110, ambavyo 51 ni vya wanawake, 53 vya vijana na tisa vya watu wenye ulemavu.

Amesema katika robo ya nne ya mwaka wa fedha, walipokea maombi kutoka vikundi 55, ambapo vikundi 34 vilipitishwa na kamati ya wataalamu kunufaika na mikopo ya Sh946 milioni katika kata 28 za wilaya hiyo.

Kauli za wanufaika

Kwa upande wake, mnufaika wa mkopo huo, Agnes Zongo amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwa mikopo hiyo imekuwa fursa ya kuboresha shughuli za kilimo cha viazi mviringo.

Naye Ester amesema pamoja na upatikanaji wa mikopo bado kuna changamoto ya ujazo wa lumbesa, hivyo ameomba Serikali iingilie kati ili wakulima waweze kunufaika na kilimo chenye tija bila kuumizwa na wafanyabiashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *