Wizara yaja na mkakati kuongeza uzalishaji umeme, majiWizara yaja na mkakati kuongeza uzalishaji umeme, maji

Unguja. Wizara ya Maji, Nishati na Madini imepanga kutekeleza bajeti yake ya Sh475.39 bilioni kwa kuzingatia vipaumbele vinane vikiwamo kuimarisha mtandao wa maji, uzalishaji wa umeme na kuendeleza matumizi ya nishati jadidifu.

Hayo yamebainishwa leo Mei 28, 2026 na Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Nadir Abdullatif wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2026/27 katika mkutano wa bajeti wa Baraza la Wawakilishi, Unguja, Zanzibar.

Waziri Nadir amesema kutokana na umuhimu wa maji wizara imepanga kuimarisha na kuongeza mtandao wa miundombinu ya usambazaji na kuongeza hifadhi ya maji kupitia ujenzi wa matangi ya kisasa ya ZincAlumn unaotumia muda mfupi zaidi ikilinganishwa na matangi ya maji ya zege.

Kuongeza mtandao wa miundombinu ya usambazaji wa maji Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na utekelezaji wa mradi wa ukarabati na uimarishaji wa miundombinu ya maji kupitia Kampuni ya NEC.

“Kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya usambazaji maji Mkoa wa Kusini Unguja katika skimu tano zikiwemo Kizimkazi, Bwejuu, Jambiani, Pagali na Cheju,” amesema Nadir

Katika mpango huo, wizara inatarajia kuanza utekelezaji wa skimu tisa za Pemba ambazo ni Pandani, Ole, Muambe-Kengeja, Madenjani, Wingwi, Chokocho, Sizini, Chambani na Wawi. Mbali na hilo pia uendelezaji wa miundombinu ya maji katika skimu saba za Pemba ambazo ni Ngwachani, Mtambwe, Junguni, Mzambarauni, Ziwani, Mjimbini, na Gombani kupitia Kampuni ya Jenkins Asia Ltd.

Pia watapambana kupunguza upotevu wa maji kwa kubadilisha mabomba chakavu na kuziba mivujo na kuendelea kusimamia ulipaji wa fidia na maandalizi ya maeneo kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Kwenye sekta ya umeme, Waziri amesema katika bajeti hii wataimarisha uzalishaji wa umeme kwa kuongeza na kuboresha vyanzo vya uhakika pamoja na kupanua na kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji ili kupunguza upotevu na kuongeza ufanisi wa huduma.

“Kuendeleza matumizi ya nishati jadidifu na teknolojia za kisasa za uhifadhi na usimamizi wa umeme, pamoja na kuboresha upatikanaji wa umeme Unguja na Pemba, ikijumuisha uimarishaji wa miundombinu ya nyaya za baharini,” amesema 

Akisoma maoni ya Kamati ya Miundombinu, Ardhi na Tehama, Mihayo Juma N’hunga amesema licha ya kazi kubwa inayofanyika katika Wizara hii hasa za kuhudumia jamii, kamati imebaini uingizwaji mdogo wa fedha za matumizi na za miradi ya maendeleo kutoka Wizara ya Fedha.

Amesema jambo hilo limesababisha kupungua kwa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu muhimu ya wizara hiyo ikiwemo kukosekana kwa usimamizi mzuri kwenye masuala ya upatikanaji wa uhakika wa maji, nishati na maliasili zisizorejesheka kwa ujumla wake.

 “Tunashauri kuwekwe mazingira rafiki na uzio kwa sehemu iliyozunguka miradi yote ya maji ili kuzuia maji ya mvua na uchafu kuzunguka matanki na visima hivyo pamoja na kuepusha uharibifu unaoweza kufanywa na wale wachache wasiokua na nia njema ya maendeleo ya nchi,” amesema Mihayo.

Pia, Kamati imeitaka wizara kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya nishati katika ngazi za mikoa, wilaya na shehia, kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na nishati jadidifu.

Kamati pia imeishauri jamii kuwa na uelewa wa kutosha kabla ya kutumia nishati hizo ili kuepusha athari zinazojitokeza mara kwa mara kutokana na kutokuwa na uelewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *