Matatizo ya Afrika yanaanzia hapa…Matatizo ya Afrika yanaanzia hapa…

Dar es Salaam. Wanazuoni wamesema Afrika imeendelea kukumbwa na matatizo mbalimbali yanayotokana na mvutano wa siasa za kimataifa.

Kauli hizo zimekuja katika kipindi ambacho Afrika inaendelea kukabiliwa na migogoro ya kisiasa, utegemezi wa kiuchumi, umaskini, maandamano ya vijana na shinikizo la mataifa makubwa duniani, unaotokana na mivutano inayoendelea katika siasa na uchumi wa dunia.

Wakizungumza katika uzinduzi wa kongamano la 17 la Kigoda cha Kiprofesa cha Mwalimu Julius Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, leo Alhamisi Mei 28, 2026, wanazuoni wameeleza tatizo kubwa la bara hilo linaanzia ndani.

Wamesema, chanzo ni namna linavyozalisha maarifa, kujitawala na kujenga umoja wake.

Katika kongamano hilo wasomi, viongozi wa chuo na wataalamu wa siasa walitafakari mustakabali wa Afrika katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi.

Afrika bado inatumia fikra za watu wengine

Akitoa mhadhara, Msemaji mkuu wa kongamano hilo, Zachariah Mampilly kutoka Chuo Kikuu cha New York, Marekani, amesema moja ya matatizo makubwa yanayoendelea kuikwamisha Afrika ni utegemezi wa maarifa na mifumo ya elimu kutoka nje.

Amesema mataifa mengi ya Afrika bado yanaendesha elimu iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni, hali inayosababisha bara hilo kushindwa kuzalisha maarifa yanayoendana na mazingira, tamaduni na mahitaji yake halisi.

 Amesema hali hiyo imeendelea kudhoofisha uwezo wa Afrika kujenga suluhisho la changamoto zake yenyewe, huku vyuo vikuu vikibaki kuwa wapokeaji wa fikra badala ya vituo vya kuzalisha mawazo mapya ya maendeleo.

Profesa Mampilly amesema pamoja na ongezeko kubwa la wanafunzi katika vyuo vikuu vya Afrika, bado uwekezaji wa elimu ya juu ni mdogo, jambo linalozifanya taasisi nyingi kushindwa kuhimili mahitaji ya kizazi kipya.

Amesema hata baada ya uhuru, Afrika haikuweza kufanya mapinduzi ya kweli katika mifumo ya elimu, isipokuwa kwa baadhi ya viongozi wachache waliotambua umuhimu wa elimu inayojitegemea.

Akimtaja Julius Nyerere, amesema miaka ya 1961 aliweka msingi wa kujenga elimu ya kujitegemea kupitia sera ya Ujamaa iliyolenga kuondoa utegemezi wa fikra kutoka nje.

Demokrasia duni na taasisi dhaifu

Mbali na elimu, Profesa Mampilly amesema ukosefu wa demokrasia na taasisi huru za kiraia umeendelea kuisukuma Afrika katika migogoro ya kisiasa na kutokuaminiana kati ya watawala na wananchi.

Alisema kukosekana kwa NGOs na asasi huru zinazoweza kuisimamia serikali kumeacha pengo kubwa la uwajibikaji katika mataifa mengi ya Afrika.

Amesema hali hiyo ndiyo inayochochea kuongezeka kwa hasira za vijana na maandamano yanayoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya nchi za Afrika, hasa kwa kizazi cha Gen Z kinachotaka uwazi, ushirikishwaji na utawala bora.

“NGOs na asasi za kiraia ni nguzo muhimu za demokrasia katika kuchochea maendeleo ya jamii,” amesema.

Amesisitiza Afrika haiwezi kujinasua katika shinikizo la mataifa makubwa bila kuwa na taasisi imara, utawala bora na mshikamano wa ndani.

Kukosekana kwa umoja

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Kigoda hicho, Alexander Makulilo amesema changamoto zinazoikabili Afrika sasa zimefanya umoja wa bara hilo kuwa jambo la lazima badala ya hiari.

Amesema fikra za Mwalimu Julius Nyerere kuhusu umoja wa Afrika bado zina uzito mkubwa kwa sababu bara hilo linaendelea kuongozwa na mifumo ya kimataifa ambayo halikushiriki kikamilifu kuitengeneza.

“Mataifa ya Afrika yanalazimika kuheshimu misingi ambayo hayakuhusika kuitunga,” amesema.

Amesema taasisi nyingi za kimataifa zimeendelea kuhubiri usawa huku zikitekeleza mifumo yenye ubaguzi dhidi ya mataifa dhaifu.

Profesa Makulilo amesema Afrika imeendelea kuwa maskini licha ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa rasilimali katika uchumi wa dunia kutokana na mifumo ya biashara isiyo na usawa.

“Hii inamaanisha Afrika lazima ijifunze kujenga viwanda vinavyojitegemea badala ya kutegemea nje,” amesema.

Amesisitiza kuwa vyuo vikuu vya Afrika havipaswi kubaki kuwa sehemu za kupokea mawazo kutoka nje, bali vinapaswa kuwa vituo vya tafiti na fikra zitakazosaidia bara kujinasua kutoka katika utegemezi.

Woga kwa wanazuoni

Aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kigoda hicho, Issa Shivji amesema uhuru wa kitaaluma katika vyuo vikuu umeendelea kubanwa, hali inayowafanya wahadhiri na wanafunzi kuogopa kusema ukweli.

Amesema mazingira hayo yanaua ubunifu wa fikra na uwezo wa kuzalisha maarifa mapya yanayoweza kuisaidia Afrika.

“Hali hii inasababisha kushindwa kuzalisha maarifa mapya,” amesema.

Shivji amesema Afrika haiwezi kushindana na nguvu za ubeberu ikiwa itaendelea kugawanyika katika mataifa madogo madogo yasiyo na mshikamano wa kisiasa na kiuchumi.

“Tuna nchi 54 Afrika kwa sasa, lakini nguvu ya ubeberu hatuwezi kushindana nayo,” amesema.

Suluhu ya kudumu

Kuhusu namna ya kuinasua Afrika katika matatizo yanayoendelea kuikabili Profesa Shivji amesisitiza ulazima wa kuvunja mipaka yake na kuunganisha nguvu za pamoja.

Amesema kuwa vijana wanapaswa kuelewa umuhimu wa umajumui wa Afrika na kushiriki katika mapambano ya kuunganisha bara.

“Bila umoja kamili wa Afrika hatuwezi kupambana na nguvu ya ukoloni mamboleo,” mesema.

Awali, akifungua kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye amesema majukwaa ya majadiliano kwa wanazuoni ni njia muhimu ya kuinasua Afrika kutoka katika matatizo yaliyopo akisema kongamano hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujadili mustakabali wa Afrika na nafasi ya fikra za Mwalimu Nyerere katika dunia ya sasa.

Amesema Afrika ya baadaye haitajengwa na kizazi kimoja, bali kwa mawazo ya pamoja ya vizazi mbalimbali vitakavyoshirikiana kutafuta majibu ya changamoto zilizopo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *