
Katibu wa muda wa swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa Marekani na Israel zinashuhudia “kudhoofika” katika eneo la Asia Magharibi. Amesisitiza kuwa vita vya siku 40 vya Ramadhani vilivyoanzishwa na tawala hizo mbili dhidi ya Iran vimedhihirisha kuwa Marekani imepoteza uwezo wa kudumisha ushawishi wake wa kisiasa katika Asia ya Magharibi.
Akihutubu katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran, Hujjatul Islam Seyyed Mohammad Hassan Abutorabifard amesema kuwa mabadiliko ya uwiano wa nguvu ni dhahiri kupitia hatua ya Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ya kujibu shambulio la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Bandar Abbas mapema Alhamisi.
Hujjatul Islam Abutorabifard amewaambia waumini kuwa, “Jeshi la vamizi la Marekani lilishambulia eneo moja katika viunga vya uwanja wa ndege wa Bandar Abbas alfajiri ya jana [Alhamisi]. Hatua hii ilitekelezwa kutokea moja ya kambi za Marekani katika ukanda huu.”
Ameongeza kuwa: “Saa kumi na dakika hamsini za alfajiri, mkono wenye nguvu wa Jeshi la Anga la IRGC ulitoa jibu kali na la kusambaratisha kwa uchokozi huo.”
Kwa mujibu wa IRGC, vikosi vyake vililenga kambi ya anga ya Marekani nchini Kuwait ikiwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio hilo la anga la Marekani karibu na mji huo wa bandari wa kusini. Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilithibitisha kuwa Iran ilifyatua kombora la balistiki kwenye kambi yake nchini Kuwait.
Hujjatul Islam Abutorabifard amesema: “Pentagon ilisema kuwa makubaliano ya usitishaji vita hayakuvunjwa, jambo ambalo linamaanisha kuwa uwiano wa nguvu umebadilika kwa manufaa ya Iran.”
Hujjatul Islam Abutorabifard, ambaye ni mwanazuoni mkongwe na mbunge wa zamani, amesema mabadilishano hayo ya kijeshi ni ushindi kwa Iran na ni ishara ya kuongezeka kwa uwezo wa Iran wa kuzuia uchokozi, ambao amesema umejengwa juu ya maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.
Aidha amebaini kuwa: “Ni lazima tusonge mbele katika mipaka ya maarifa, teknolojia, na nguvu za ulinzi, kwani nguvu hii ndiyo iliyoifedhehesha Marekani.” Aidha amesisitiza kuwa, “Leo hii, ulimwengu unaelewa lugha moja tu: lugha ya nguvu.” Halikadhalika amesema uwezo wa kijeshi wa Iran kama matokeo ya mafanikio ya kisayansi yaliyojikita katika imani.
Mwanazuoni huyo ametoa wito wa kuimarisha “mamlaka ya watu wa Iran na Mhimili wa Muqawama (Axis of Resistance),” akiongeza kuwa njia ya kufikia hili ni kupanua uwezo wa taifa.
Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa Tehran aidha amekemea mashambulizi “ya kikatili” ya Israel nchini Lebanon, ambayo alisema yamesababisha uharibifu mkubwa.
