
Siha. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kuwalinda na kuwaheshimu wazee kwa kutambua mchango wao mkubwa katika historia ya taifa na maendeleo ya nchi, kikieleza kuwa wazee ni hazina ya hekima inayopaswa kuthaminiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Mei 29,2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Sanya Juu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Kihongosi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakibeza CCM kwa kukiita chama cha wazee, lakini akasema chama hicho kinajivunia kuwa na wazee kutokana na mchango wao mkubwa kwa taifa.
“Wengine wanasema CCM ni chama cha wazee, ndiyo ni chama cha wazee. Ukiona chama hakina wazee ni kigenge cha wahuni. Wazee wana hekima, wanajua nchi ilipotoka, ilipo na inapokwenda. Bila wazee tungepata uhuru?” alihoji Kihongosi
Amesema CCM haitaruhusu tabia ya kuwadharau wazee na kwamba itaendelea kuwatetea na kuwalinda kwa nguvu zote kwa sababu wana nafasi kubwa katika jamii na taifa kwa ujumla.
“Leo tunapata wapi ujasiri wa kutukana wazee? Wazee wetu tutawaheshimu na kuwalinda kwa nguvu zote. CCM inatambua kazi yao kubwa ndani ya nchi hii,” amesema.
Katika hotuba yake, Kihongosi amesema CCM itaendelea kuwa chama kinachoongoza nchini kutokana na kuungwa mkono na wananchi kupitia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni upatikanaji wa umeme vijijini, ujenzi wa vituo vya afya, shule, madarasa na barabara katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tukisema umeme kila kijiji unawaka, vituo vya afya vinajengwa, barabara zinajengwa, madarasa na shule zinajengwa, sasa kwanini tusishinde uchaguzi?” alisema.
Kihongosi amesema nguvu ya CCM inatokana na kuwa karibu na wananchi kupitia mfumo wa mashina na mabalozi wa nyumba kumi, akieleza kuwa chama hicho huendesha kampeni zake kwa kuwafikia wananchi mmoja mmoja.
“Sisi ni mabingwa wa kutafuta kura. Tunaomba kura mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba, mpaka vijiweni na vilabuni tunaenda kuomba kura kwa unyenyekevu,” amesema.
Aidha, aliwataka wananchi wa Siha kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akisema maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani.
“Amani ni muhimu sana. Bila amani hakuna mradi wa maendeleo utakaotekelezwa. Masoko yatafungwa, watu hawataenda mashambani wala kufanya shughuli zao za kila siku,” amesema.
Aliwataka wananchi kutosikiliza watu wanaohamasisha vurugu na maandamano kwa maslahi yao ya kisiasa huku wao wakiwa salama nje ya maeneo husika.
“Mtu anakwambia choma kituo cha polisi, ukikichoma utalindwa na nani? Kabla hujafanya uamuzi changanya na akili yako. Wanaowahamasisha kufanya fujo wengine hata hawapo hapa Siha, lakini nyie ndiyo mnaoishi hapa, mtazaliwa hapa na mtazikwa hapa,” amesema.
Kihongosi pia alisisitiza umuhimu wa kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama akisema askari wanafanya kazi kubwa ya kulinda maisha ya wananchi na mali zao.
“Mtu anayekwambia uchukie polisi hakutakii mema. Askari ndiyo wanalinda usalama wetu, maduka yetu na miundombinu ya taifa. Vyombo vya ulinzi na usalama lazima viheshimiwe na kuombewa,” amesema.
Aliongeza kuwa baadhi ya vyama vya upinzani vinafanya vurugu kama sehemu ya kujijenga kisiasa, lakini CCM itaendelea kuwa imara kutokana na kazi inayofanya kwa wananchi.
“Sisi tunawasubiri 2030. Wananchi wataamua kwa kuangalia nani amefanya kazi na nani hajafanya,” amesema
