Muungano wa Madaktari Kenya waipa serikali masaa 48, wapinga wagonjwa wa Ebola Marekani kutumwa KenyaMuungano wa Madaktari Kenya waipa serikali masaa 48, wapinga wagonjwa wa Ebola Marekani kutumwa Kenya

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU) umepatia serikali muda wa saa 48 kueleza hadharani masharti kamili ya makubaliano yake na Marekani au ikabiliwe na mgomo wa kitaifa wa madaktari.

Ni baada ya kutangazwa kwamba, wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka Marekani wamewasili nchini Kenya na tayari wanaendelea na maandalizi ya kituo maalumu cha Ebola ambacho Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesema kitaanza kufanya kazi ndani ya siku saba zijazo.

Kwa mujibu wa vyanzo, kituo hicho kinajengwa karibu na maeneo ya kijeshi ya Uingereza katika Kaunti ya Laikipia.

Lengo lake limetajwa kuwa ni kwa ajili ya kuwatenga raia wa Marekani walioathiriwa au waliokaribiana na virusi vya Ebola.

Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Davji Bhimji Atellah, amesema kituo hicho kinaanzishwa katika Kituo cha Anga cha Laikipia.

“Kenya ni taifa huru, si eneo la kutengwa wagonjwa wa magonjwa hatari kwa maslahi ya kisiasa,” amesema Dkt Atellah.

“Hatutakubali Kenya kutumiwa kama mahali pa kuhifadhi wagonjwa wa virusi hatari ambavyo havikutoka nchi yetu.”

Muungano huo umeitaka serikali kueleza kwa nini Kenya imechaguliwa kupokea raia wa Marekani walio na Ebola ilhali mataifa jirani na maeneo yaliyoathirika zaidi hayajapewa jukumu hilo.

“Ikiwa Amerika inaamini safari ya saa 12 ya kuwarudisha raia wake Washington ni hatari sana, kwa mantiki gani ni salama kuwaleta Kenya?” alihoji Dkt Atellah.

Muungano huo pia umesema hautakubali mfumo wa afya wa kibaguzi nchini Kenya.

KMPDU imesema haitakubali madaktari wa Kenya kutumiwa kama wafanyakazi wa bei rahisi katika mazingira hatari bila mishahara bora, marupurupu ya kazi hatari na bima kamili ya afya.

Wakati huo huo, Wizara ya Afya kupitia Katibu katika Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni ilisema Kenya ina uhuru wa kushirikiana na mataifa mengine katika kupambana na Ebola iliyosababisha zaidi ya vifo 100 nchini DRC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *