
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Alkhamisi ya jana aliwasilisha ripoti yake ya kila mwaka kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, ambayo inarekodi ukiukwaji mkubwa na wa kutisha wa sheria uliofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
Guterres amesema Umoja wa Mataifa umerekodi mifumo inayoendelea ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya Wapalestina wanaoshikiliwa huko Israel na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu wakati wa kuwa kizuizini na katika mahojiano mwaka wa 2025.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vikosi vya jeshi la Israel vimejumuishwa kwenye orodha nyeusi ya Umoja wa Mataifa ya wahusika wa unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba vikosi vya Israel na askari usalama wametekeleza uhalifu wa kingono dhidi ya wafungwa wa Kipalestina – wakiwemo wanaume, wanawake na watoto – wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na ubakaji, ubakaji wa genge na ukatili unaolenga sehemu za siri.
Guterres amelaani kushindwa serikali ya Israel kuchunguza ukiukwaji huo wa sheria na kuwawajibisha wale waliohusika. Amesema kwamba kufutwa mashtaka dhidi ya wanajeshi waliohusika katika uhalifu makubwa katika kambi ya Sde Teiman kunaendeleza hali ya kukwepa adhabu baada ya kuhusika na unyanyasaji wa kingono.
Baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesisitiza tena ombi lake kwa Israel “kusitisha mara moja vitendo vyote vya unyanyasaji wa kingono na kuruhusu vyombo vya Umoja wa Mataifa kupata ruhusa ya kuchunguza uhalifu huo bila vikwazo.”
Mnamo Aprili 21, Umoja wa Mataifa ulinukuu ripoti ya haki za binadamu inayowaorodhesha walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wakitumia mbinu za “ukatili, unyanyasaji wa kingono na vitisho” dhidi ya Wapalestina.
Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisema kwamba ripoti iliyoandaliwa na Baraza la Wakimbizi la Norway ilionyesha kwamba Wapalestina – hata ndani ya nyumba zao – walinyanyaswa kingono na kukabiliwa na vitisho kutoka kwa walowezi wa Kizayuni.
