Dar es Salaam. Wakati hamasa ya michuano ya Kombe la Dunia ikiendelea kushika kasi huku mataifa mbalimbali yakitangaza vikosi vyao vya mwisho neema imeendelea kuwa upande wa wadau na mashabiki wa soka nchini.

Kampuni ya Mixx imewakabidhi zawadi washindi wa awamu ya kwanza wa kampeni ya “Kila muamala ni bao la ushindi”, inayolenga kuunganisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali na burudani ya soka.

Kampeni hiyo, inayofanyika kwa ushirikiano na Hisense chini ya kauli mbiu “Ikiingia tu goli”, imekuwa ikiwapa watumiaji wa Mixx Super App nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali kupitia miamala ya kila siku.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi hizo, Mkuu wa Kitengo cha Chapa na Mawasiliano wa Mixx, Anisah Mamuya, alisema kampeni hiyo imejengwa kutokana na mapenzi makubwa ya Watanzania kwa mchezo wa soka na uwezo wake wa kuchochea matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.

Alisema Kombe la Dunia ni tukio linalounganisha mamilioni ya watu duniani, hivyo kampeni hiyo inalenga kuwapa Watanzania nafasi ya kushiriki msisimko huo huku wakinufaika na zawadi mbalimbali.

Katika droo ya kwanza ya kampeni hiyo, washindi saba walijishindia shilingi milioni moja kila mmoja, ambapo watano walitoka Dar es Salaam ambao ni Yango Kasagamba, Asha Mohamed, Juma Ally, Rehema Said na Said Bakari na wawili kutoka mikoa ya Pwani, Fatuma Juma na Tanga, Musa Abdallah. Mmoja wa washindi, Kasagamba ambaye ni mjasiriamali, alisema fedha alizoshinda zitamsaidia kuongeza mtaji wa biashara na kugharamia mahitaji ya familia.

Washindi wengine watatu walijinyakulia vifaa vya kielektroniki kutoka Hisense, ikiwemo televisheni, friji na spika, wakitoka Dar es Salaam, Zanzibar na Tanga.

 Mamuya alibainisha kuwa kampeni hiyo bado inaendelea, ambapo washiriki wengine wanaendelea kupata nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali, ikiwemo safari ya kwenda Mexico kushuhudia mechi za Kombe la Dunia mubashara pamoja na zawadi kuu ya shilingi 50 milioni  itakayotolewa mwishoni mwa kampeni.

Kampeni ya “Kila muamala ni bao la ushindi” inalenga pia kuhamasisha matumizi ya Mixx Super App katika huduma za kifedha kama kutuma na kupokea fedha, kulipa bili na kufanya malipo kwa njia ya Lipa kwa Simu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *