Dar es Salaam. Safari ya miaka 72 ya maisha ya duniani ya Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa, inatarajiwa kuhitimishwa leo, katika makaburi ya Kondo, jijini Dar es Salaam.

LIVE: Mwisho wa enzi za Leonard Mususa

Mususa, aliyeitumikia MCL inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, alifariki Dunia Mei 30, mwaka huu na msiba wake umefanyika nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi, walitembelea nyumbani kwake, kuungana na waombolezaji kuhudhuria msiba huo nyumbani kwa marehemu Mususa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa MCL, Bakari Machumu, akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu Leonard Mususa, aliyefariki Dunia Mei 30, 2026. 

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi ya Mususa iliyotolewa na familia yake, atazikwa leo katika makaburi ya Kondo jijini Dar es Salaam, baada ya ibada maalumu katika Kanisa la St. Peter jijini humo.

Kwa upande wa Serikali, waliotembelea nyumbani hapo, Masaki jijini Dar es Salaam, ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa MCL.

Machumu, alifika msibani usiku wa juzi, akiambatana na waombolezaji wengine. Pia, alikuwepo Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga.

Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga.

Balozi Ulanga pia, alikuwa sehemu ya bodi ya MCL chini ya Mususa. Alikuwa mjumbe wa bodi hiyo, kabla ya baadaye kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa balozi.

Sambamba na hao, wageni wengine waliofika nyumbani hapo kwa Mususa ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalyn Mworia, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Magazeti la Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, Mpoki Thomson na watumishi wengine wa kampuni hiyo.

Ndugu na jamaa wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Leonard Mususa, baada ya mwili kuwasili nyumbani kwake jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga.

Jana mwili wake ulipokelewa nyumbani kwake Masaki, saa 9:29 alasiri, ratiba iliyofuatiwa na misa maalumu iliyofanyika nyumbani hapo.

Leo, ratiba itaanza na chai kisha ibada katika Kanisa la St. Peter, itafuatiwa na utoaji heshima za mwisho na safari ya kwenda makaburi ya Kondo kwa ajili ya maziko itafuata.

Huyu ndiye Mususa

Mususa alifahamika zaidi ya taaluma yake ya uhasibu na anatajwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Akizaliwa Septemba 25, mwaka 1953 katika visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza, eneo ambalo alipata elimu yake ya msingi na baadaye kujiunga na Sekondari katika Shule ya Sekondari Kibaha.

Mususa ambaye ni mtoto wa pili kati ya saba wa wazazi wake, alisoma Chuo Kikuu nchini Uingereza na alipomaliza alipata nafasi ya kuwa Mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa takriban mwaka mmoja.

Baadaye, akahamia katika Kampuni ya Ukaguzi ya Price House Water Coopers Ltd, ilivyokuwa inawakilisha Afrika Kusini, Uingereza na Tanzania na alistaafu mwaka 2014 baada ya kuhudumu kwa takriban miaka 36.

Pia, Mususa ni mmoja wa waasisi wa CEO Roundtable alihudumu kwa nafasi ya Mwenyekiti wa bodi kwa miaka 10 na aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mifumo ya Kodi akiteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *