
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya kuwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinawasukuma mamilioni ya watu duniani kuingia katika hali ya njaa huku bara Afrika likionekana kuathirika zaidi.
Ripoti iliyochapishwa na Shirika la Habari la Umoja wa Mataifa imesema: “Kile kilichoanza takribani siku 100 zilizopita kama mgogoro wa kijiografia na kisiasa katika Mashariki ya Kati sasa kinazidi kubadilika kuwa mgogoro wa usalama wa chakula katika maeneo mengine ya dunia. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuhusu kuongezeka kwa njaa barani Afrika, huku watoto walioathiriwa na utapiamlo wakiongezeka Afghanistan.”
Habari hiyo ilionya kuwa hatari ya janga la kibinadamu inaelea juu ya maeneo mengi kutokana na kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji duniani, hali inayotokana na vita visivyo na msingi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Ripoti hiyo imebaini kuwa, “Licha ya kuwepo kwa usitishaji dhaifu wa mapigano kati ya Marekani na Iran, mapigano ya hapa na pale pamoja na hali ya kutokuwa na uhakika katika Mlango-Bahari wa Hormuz vinaendelea kuathiri minyororo ya usambazaji ya kimataifa. Hali hii inasababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji na mafuta, na kuongeza mzigo kwa operesheni za misaada ya kibinadamu ambazo tayari zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa ufadhili.”
WFP inakadiria kuwa watu milioni 45 wanaweza kuingia katika hali ya ukosefu mkali wa usalama wa chakula ikiwa mzozo huo utaendelea na bei ya mafuta itaendelea kubaki karibu dola 100 kwa pipa hadi mwezi Julai.
Shirika hilo pia limeeleza wasiwasi kuwa watu wengine milioni 45 wanaweza kusukumwa zaidi katika njaa kutokana na uhusiano wa karibu uliopo kati ya bei za nishati na bei za chakula.
WFP imesema tayari shinikizo linaongezeka, na imetoa onyo kali kuhusu hali hiyo.
Akizungumza katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau, amesema tahadhari zilizotolewa mapema wakati mgogoro huo ulipoanza kuhusu athari za kupanda kwa bei za nishati sasa zinaanza kujidhihirisha katika baadhi ya nchi zilizo hatarini zaidi duniani.
WFP imeonya kuwa watu wengine milioni 2.5 nchini Somalia tayari wameingia katika hali ya ukosefu shadidi wa chakula. Aidha, watu milioni 2.3 zaidi nchini Afghanistan na wengine milioni 1.3 nchini Sri Lanka pia wamesukumwa katika njaa kali.
Skau amesema kuwa sababu zinazosababisha hali hiyo hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Hata hivyo kwa ujumla, kupanda kwa bei za chakula, pamoja na ukosefu wa ufadhili wa kutosha kwa operesheni za kibinadamu na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, kunapunguza idadi ya watu ambao mashirika ya misaada yanaweza kuwafikia kwa rasilimali zilizopo.
Kwa mtazamo wa muda mrefu, Skau ameonya kuwa hali inaweza kuwa ngumu zaidi. Amesema gharama kubwa za mbolea zinaweza kupunguza uzalishaji wa kilimo katika Afrika Mashariki wakati wa msimu ujao wa upandaji, jambo ambalo linaweza kusababisha upungufu mkubwa wa chakula katika miezi ijayo.