
Dunia inapoadhimisha Siku hii ya Kimataifa (IAAD) ambayo kila mwaka huwa tarehe 13 Juni, watetezi wa haki za binadamu wanatoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi kupambana na ubaguzi unaotokana na rangi ya ngozi na kuhakikisha haki, usalama na ustawi wa watu wenye ualbino.
Kaulimbiu ya mwaka huu, inaangazia ubaguzi wa kila siku ambao watu wenye ualbino bado wanakumbana nao pamoja na athari zake kwa afya ya akili, kujiamini na ushirikishwaji katika jamii.
“Ubaguzi unaotokana na rangi ya ngozi mara nyingi hudharauliwa kana kwamba hauna madhara, lakini athari zake ni za kweli na hudumu kwa muda mrefu,” wamesema waandaaji wa kampeni yam waka huu wakiongeza kuwa “Hakuna mtu anayepaswa kuvumilia dhihaka, kutengwa au kudhalilishwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yake.”
Ubaguzi wa kila siku huacha majeraha ya kudumu
Watetezi wa haki za watu wenye ualbino wanasema kuwa ubaguzi unaweza kujitokeza kwa namna mbalimbali, ikiwemo kutazamwa kwa muda mrefu, kutolewa maoni ya kejeli, kunyanyaswa, kutengwa kijamii na kuhusishwa na dhana potofu.
Ingawa vitendo hivyo vinaweza kuonekana vidogo kwa baadhi ya watu, wataalamu wanaonya kuwa uzoefu wa mara kwa mara wa ubaguzi unaweza kusababisha madhara makubwa ya kihisia na kisaikolojia, hasa kwa watoto na vijana wanaojenga utambulisho wao na kujiamini.
“Kila mtoto anastahili kukua akiwa anajihisi kuthaminiwa, kuheshimiwa na kujivunia alivyo,” waandaaji wamesema. “Jamii inapokubali ubaguzi kuwa jambo la kawaida, huathiri kujiamini, utu na hisia za kuwa sehemu ya jamii.”
Kampeni ya mwaka 2026 inasisitiza kwamba kusherehekea rangi zote za ngozi si suala la kukubalika tu bali pia ni suala la haki za binadamu.
Haki za binadamu ndizo kiini cha kampeni
Kwa mujibu wa mifumo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, ubaguzi unaotokana na rangi au asili ya mtu unadhoofisha haki ya mtu kufurahia fursa sawa, usalama na ushiriki kamili katika jamii.
“Ujumbe wa ‘Ninajivunia Ngozi Yangu’ unahusu utu wa binadamu kwa msingi wake,” watetezi wameeleza. “Ni kuhusu kutambua ubinadamu, thamani na haki sawa za kila mtu bila kujali rangi ya ngozi au tofauti za kijenetiki.”
Viongozi wa kampeni wanazihimiza serikali, taasisi na jamii kuchukua hatua dhidi ya chuki na ubaguzi, kusikiliza sauti za watu wenye ualbino na kujenga mazingira salama na jumuishi kwa wote.
Ualbino ni nini?
Ualbino ni hali ya nadra ya kurithi inayopatikana tangu kuzaliwa. Hali hii hutokea pale mwili unapozalisha kiwango kidogo sana au kutokuzalisha kabisa melanini, rangi inayotoa mwonekano wa ngozi, nywele na macho.
Ualbino huwapata watu wa makabila yote, jinsia zote na katika nchi zote duniani.
Kutokana na ukosefu wa melanini, watu wengi wenye ualbino hupata changamoto za kuona na huwa katika hatari kubwa ya kuathiriwa na miale ya jua pamoja na kupata saratani ya ngozi.
“Hakuna tiba ya kurejesha melanini mwilini,” wataalamu wa afya wanaeleza. “Kinachookoa maisha ni upatikanaji wa huduma za afya, mafuta ya kujikinga na jua, miwani ya jua, mavazi ya kujikinga na uchunguzi wa mara kwa mara wa afya.”
Inakadiriwa kuwa katika Amerika Kaskazini na Ulaya, mtu mmoja kati ya watu 17,000 hadi 20,000 ana aina fulani ya ualbino. Hata hivyo, kiwango hicho ni kikubwa zaidi katika baadhi ya nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania na Zimbabwe.
Hatari zinazozuilika bado zinahatarisha maisha
Licha ya kuwepo kwa njia za kujikinga, saratani ya ngozi bado ni moja ya vitisho vikubwa kwa watu wenye ualbino.
Katika baadhi ya nchi, idadi kubwa ya watu wenye ualbino hufariki dunia kutokana na saratani ya ngozi kati ya umri wa miaka 30 na 40 kwa sababu ya ukosefu wa huduma muhimu za kinga na matibabu.
“Saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino inaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa,” watetezi wamesisitiza. “Hakuna mtu anayepaswa kupoteza maisha kwa sababu tu hana uwezo wa kupata mafuta ya kujikinga na jua, huduma za afya au vifaa vya kujikinga.”
Wanaharakati wanasema watu wenye ualbino ni miongoni mwa makundi yanayoendelea kuachwa nyuma katika maendeleo na wanapaswa kupewa kipaumbele katika mipango ya afya ya umma na haki za binadamu.
Wito wa ushirikishwaji na heshima
Mbali na changamoto za kiafya, watu wenye ualbino mara nyingi hukabiliwa na aina nyingi za ubaguzi zinazotokana na ulemavu wa kuona na rangi yao ya ngozi.
Siku ya Kimataifa ya Uelimishaji kuhusu Ualbino 2026 inapoadhimishwa duniani kote, waandaaji wa kampeni wanawahimiza wananchi, shule, sehemu za kazi na serikali kupinga dhana potofu na kukuza ushirikishwaji.
“Lazima tuhame kutoka kwenye uhamasishaji kwenda kwenye hatua za vitendo,” waandaaji wamesema. “Kwa kupambana na ubaguzi na kusherehekea tofauti zetu, tunaweza kujenga jamii ambazo kila mtu anaishi kwa usalama, heshima na kujivunia ngozi yake.”
Maadhimisho ya mwaka 2026 yanahitimishwa kwa ujumbe mmoja wenye nguvu, kila rangi ya ngozi inastahili utu, usawa na heshima.