‎Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Issa ametaka kufanyika mjadala wa kitaifa kuhusu umuhimu wa wafanyakazi wa majumbani ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wao katika maendeleo ya familia na kuimarisha mazingira bora ya kazi kwa waajiri na waajiriwa.

‎Akizungumza leo Juni 13, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Programu ya Kutetea Wafanyakazi wa Majumbani (Empowered II), Zainabu amesema wafanyakazi wa majumbani ni nguzo muhimu ya ustawi wa familia nyingi nchini na wanapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa.

‎“Tunahitaji kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu umuhimu wa wafanyakazi wa majumbani. Hili ni jambo linalopaswa kuendelea kufanyika ili wale wanaowaajiri watambue kuwa wanawaajiri watu muhimu sana ambao ni msingi wa maendeleo ya familia zetu,” amesema Zainabu.

‎Amesema pamoja na umuhimu wa kuwaelimisha waajiri kuhusu mchango wa wafanyakazi wa majumbani, ni lazima wafanyakazi hao pia wajengewe uwezo ili watambue wajibu wao na kuongeza weledi katika kazi wanazozifanya.

‎Kwa mujibu wa mbunge huyo, wafanyakazi wa majumbani ni sehemu muhimu ya maendeleo ya familia na uchumi, hivyo mijadala inayohusu sekta hiyo inapaswa kuzingatia maslahi ya waajiri na waajiriwa kwa pamoja.

‎Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna changamoto zinazochangia migogoro katika maeneo ya kazi, ikiwemo baadhi ya wafanyakazi kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

‎Amesema baadhi ya waajiri wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa nidhamu, kutowajibika na matumizi ya simu wakati wa kazi, hali inayodhoofisha utendaji na kuathiri mahusiano kazini.

‎“Tunapozungumzia haki za wafanyakazi wa majumbani ni lazima pia tuzungumzie wajibu wao. Elimu inapaswa kutolewa kwa pande zote ili kujenga mahusiano bora kati ya waajiri na waajiriwa,” amesema.

‎Aidha, amesema mjadala wa kitaifa utatoa fursa ya kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa majumbani na waajiri wao, pamoja na kutafuta suluhisho la kuboresha mazingira ya kazi nchini.

‎Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Hoteli, Majumbani na Taasisi Zinazofanana Tanzania (Chodawu), Said Wamba, amesema Programu ya Empowered II itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika mikoa 14, hatua itakayoongeza idadi ya mikoa iliyofikiwa na mradi huo kufikia 21, ikijumuisha mikoa saba iliyofikiwa katika awamu ya kwanza.

‎Wamba amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza ulizaa matokeo chanya kwa kuwawezesha wafanyakazi wengi kupata elimu na ujuzi uliowasaidia kuboresha maslahi yao na maendeleo ya maisha yao.

‎“Lengo letu ni kuhakikisha wafanyakazi wa majumbani wanaheshimika kama ilivyo katika sekta nyingine za kazi kwa kulipwa mishahara inayolingana na thamani ya kazi wanayoifanya na inayoweza kubadilisha maisha yao,” amesema Wamba.

‎Ameeleza kuwa baadhi ya wafanyakazi waliopata mafunzo na kujiendeleza kielimu hadi ngazi ya stashahada wamefanikiwa kupata mishahara bora zaidi kutokana na ongezeko la ujuzi na weledi wao.

‎Naye mfanyakazi wa majumbani mwenye uzoefu wa kufanya kazi nje ya nchi, Amina Hajji, amesema wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi katika mataifa ya kigeni wanapaswa kujifunza lugha za nchi wanazokwenda ili kuboresha mawasiliano na kuongeza fursa za kupata mishahara mizuri.

‎Amesema uwezo wa kuzungumza lugha za waajiri huwapa wafanyakazi nafasi kubwa ya kunufaika zaidi na ajira hizo kuliko wenzao wasiokuwa na ujuzi huo.

‎“Tunawaomba mawakala wetu watusaidie kupata mafunzo ya lugha za nchi tunazokwenda kufanya kazi hata kama tutachangia gharama zake, ili tuweze kushindana na kupata malipo bora kama wafanyakazi kutoka mataifa mengine,” amesema Amina.

‎Mradi wa Empowered II unafadhiliwa na Shirika la CVM kwa kushirikiana na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania kwa lengo la kuendeleza utetezi wa haki na maslahi ya wafanyakazi wa majumbani nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *