Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametangaza siku ya Jumatano Juni 17, 2026 kuwa ya mapumziko ili kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu 1448 Hijiria.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Juni 15, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed, Rais Mwinyi ametoa tamko hilo leo Jumatatu Juni 15, 2026 Ikulu Zanzibar.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa uamuzi wa Serikali wa kuutambua mwaka mpya wa Kiislamu kuwa miongoni mwa siku muhimu Zanzibar.

“Siku hiyo itatoa fursa kwa wananchi hususani waumini wa dini ya Kiislamu kuukaribisha mwaka mpya kwa ibada dua, na matendo mema pamoja na kumuomba mwenyezi Mungu aendelee kujaalia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla amani, umoja na ustawi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo. Dk Mwinyi amewataka wananchi kuutumia mwaka mpya kwa kujitathimini na kuimarisha uchaMungu, kusaidiana na kuendeleza maadili mema yanayojenga familia na taifa lenye mshikamano.

Pia, amezitaka taasisi za Serikali, waajiri na wananchi wote kuzingatia tangazo hilo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Ametumia fursa hiyo kuwatakia Waislamu na wananchi wote heri ya mwaka mpya wa Kiislamu 1448 Hijiria, akimuomba Mwenyezi Mungu aufanye kuwa mwaka wa kheri, amani, afya njema na maendeleo kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *