
Wananchi nchini wametakiwa kusoma na kuelewa mikataba ya huduma za umeme na maji wanayosaini na watoa huduma ili kujilinda dhidi ya changamoto za bili hewa na migogoro inayoweza kujitokeza katika malipo ya huduma hizo.
Wito huo umetolewa Juni 19, 2026 na Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wilfred Mwakalosi, wakati wa semina maalumu iliyowakutanisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Lindi, maofisa tarafa pamoja na watendaji wa kata kutoka Manispaa ya Lindi.
Semina hiyo ililenga kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi ya msingi ili waweze kushughulikia kwa haraka na kwa ufanisi kero za wananchi zinazotokana na huduma za nishati na maji, sambamba na kuelewa taratibu sahihi za kushughulikia malalamiko.
Akizungumza katika semina hiyo, Mwakalosi amesema wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia bili kubwa zisizoeleweka, hali inayotokana na kutokujua haki zao katika mikataba ya huduma, hivyo kusisitiza umuhimu wa kusoma na kuelewa kabla ya kusaini mikataba hiyo.
“Wananchi wengi wanalalamika kurundikiwa bili kubwa, lakini wakifuatilia unakuta hawajui hata haki zao za msingi kwenye mkataba,tunasisitiza, soma mkataba kabla hujasaini,” amesema Mwakalosi
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuhifadhi risiti za malipo kama ushahidi muhimu utakaosaidia pindi panapotokea migogoro ya bili au makadirio yasiyo sahihi ya matumizi ya huduma.
Ameongeza kuwa EWURA imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali yakiwemo bili za makadirio, kukatwa huduma bila taarifa pamoja na changamoto za ubora wa bidhaa, akibainisha kuwa bila ushahidi na uelewa wa mkataba, ni vigumu kwa mteja kushinda kesi hata kama ana haki.
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa Seaview, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Lindi, Twahili Mpuluji, aliwataka watoa huduma wa nishati na maji kutimiza wajibu wao wa kisheria kwa kutoa huduma bora na kwa wakati pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na mamlaka husika.
“Huduma ya umeme na maji ni haki ya msingi, mtoa huduma asipotoa taarifa sahihi za mgao, za bili au za hitilafu, anakiuka haki ya mwananchi, tutashirikiana na EWURA kuhakikisha kila mwananchi wa Lindi anapata huduma inayostahili,” amesma Mpuluji.
Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki wa EWURA, Lorivii Long’idu, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa serikali za mitaa ili waweze kutatua changamoto ndogo ndogo kabla hazijafika ngazi za juu, na hivyo kupunguza malalamiko kwa wananchi.
Kwa upande wake, Hadija Mbango, mtendaji wa Kata ya Mipingo, amesema semina hiyo imewapa uelewa mpya wa namna ya kupokea, kusajili na kufuatilia malalamiko ya wananchi kwa mujibu wa sheria, na kuahidi kusambaza elimu hiyo hadi ngazi ya vitongoji ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.