
Moshi. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan tayari amezindua jengo la tiba mionzi katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini, KCMC lililogharimu zaidi ya Sh17 bilioni.
Jengo hilo, lenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,500 kwa mwaka, liliwekewa jiwe la msingi na Rais Samia mwaka 2021 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo.
Uzinduzi wa jengo hilo unatarajiwa kutoa ahueni kwa mamia ya wagonjwa wa saratani ambao hapo awali walilazimika kupewa rufaa kutoka KCMC kwenda kupata huduma za tiba ya mionzi katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuzindua jengo hilo, Rais Samia amepanda mti wa matunda katika hospitali hiyo kama moja ya kumbukukumbu ya uzinduzi huo.
Aidha, Rais Samia ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, wakiwemo mawaziri, wakuu wa wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, wakuu wa idara za serikali na taasisi za umma, pamoja na viongozi wa dini mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga, hospitali hiyo huhudumia wagonjwa wa saratani 9,446 kwa mwaka, huku wastani wa wagonjwa wapya ukiwa 900 kila mwaka.
Profesa Masenga amesema kuwa takribani asilimia 65 ya wagonjwa hao huhitaji huduma za tiba ya mionzi, na hivyo walilazimika kusafiri kwenda Hospitali ya Ocean Road kwa ajili ya matibabu hayo.
Aidha, Profesa Masenga alisema kuwa baadhi ya wagonjwa walikuwa wakishindwa kumudu gharama za usafiri, malazi na mahitaji mengine ya kujikimu, jambo linaloweza kuchelewesha matibabu, kuongeza makali ya ugonjwa na kusababisha vifo ambavyo vingeepukika.
Uzinduzi wa jengo hilo unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu ya saratani kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo jirani, huku ukipunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.