
Dar es Salaam. Hatimaye daladala zinazofanya safari zake Barabara ya Kilwa zimeanza kuingia katika kituo cha mabasi yaendayo haraka, maarufu mwendokasi Mbagala ikiwa ni ishara ya kutekeleza agizo lililotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Juni 15, 2026.
Katika agizo hilo lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo, aliyesema wananchi wanaotoka maeneo ya Mkuranga, Toangoma na vitongoji vingine watashuka katika Kituo cha Mbagala Rangitatu na kuunganisha safari zao kwa kutumia mabasi ya mwendokasi kwenda katikati ya jiji na maeneo mengine, utekelezaji ambao ulipaswa kuanza leo, Jumatano, Julai 1, 2026.
Pia gari za ruti nyingine zinazotumia barabara hiyo, hazitatakiwa kushusha wala kupakia abiria vituo vya katikati hadi zifike mwisho wa safari.
Uamuzi huo wa Latra unakuja ikiwa imepita miezi mitatu tangu mtoa huduma wa mabasi hayo, Kampuni ya Mofat, ilalamikie kukosa faida ya uwekezaji wake, ikisisitiza kuwa uwepo wa daladala unafanya mabasi yake kutoa huduma chini ya uwezo wake.
Mofat ina mabasi 200 lakini kwa sasa 50 pekee ndiyo yanayoelezwa na uongozi kuwa yanayofanya kazi huku mengine 150 yakiwa yameegeshwa jambo ambalo ni hasara kwao.
Hata hivyo, Mwananchi ilifika katika maeneo hayo kuanzia saa 1:00 asubuhi na kupiga kambi hapo hadi saa 4:00 asubuhi bila kuona daladala yoyote ikiwa imeingia.
Kutokana na hilo, ilimpigia Kaimu Meneja Leseni, Ngereza Patel, ambaye alikiri hilo kutokea na kueleza wanalifuatilia na angerudi na majibu.
Hata hivyo, ilipofika saa 6:57 mchana, meneja huyo alimueleza mwandishi wa habari hii kuwa gari hizo zimeshaanza kutekeleza agizo hilo kwa kuingia kituoni hapo kwa usimamizi na maelekezo ya maofisa wa Latra.
Hata hivyo, kwa daladala ambazo bado zinapakia na kushusha vituo vya katikati, Patel amesema hilo litamalizika taratibu kwa kuwa bado wanaendelea kutoa elimu kwa madereva.
Walichosema wananchi
Wakizungumza kuhusu hatua hiyo baadhi ya wadau akiwemo dereva wa daladala, Norbert Mdege, amesema wanashukuru Serikali kuwaletea mwendokasi kwani wameleta unafuu wa usafiri pia kwa abiria.
Mdege amesema kikubwa katika hilo daladala wanalisha mwendokasi na mwendokasi inawalisha daladala na kubainisha kuwa kitu chochote kinapoanza inakuwa ngumu kulipokea ila baadaye anaamini watazoea.
Mmoja wa wananchi, Marietha Joseph, amesema urahisi wanaoupata katika hilo ni kwamba unashuka kwenye daladala na kwenda kwenye mwendokasi hapohapo.
Naye Khlafan Said amesema utaratibu huo ni mzuri kwa kuwa utawapunguzia kutembea umbali mrefu kuzifuata daladala eneo jingine.