Arusha. Serikali imesema sasa ni wakati wa kuhamisha nguvu kutoka kwenye kupunguza maambukizi ya kipindupindu na kuelekeza mikakati katika kukitokomeza kabisa ugonjwa huo nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, amesema hatua hiyo inawezekana kupitia ushirikiano wa Serikali, wananchi na wadau mbalimbali pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya maji safi, vyoo bora na maeneo ya kunawia mikono.

Profesa Shemdoe ameyasema hayo leo Julai Mosi, 2026 jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathmini ya utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira kwa ngazi ya mikoa na halmashauri Tanzania Bara.

Amesema takwimu zinaonyesha mafanikio katika mapambano dhidi ya kipindupindu baada ya idadi ya wagonjwa kupungua kutoka zaidi ya 12,000 hadi takribani 700 mwaka uliopita.

Kutokana na mafanikio hayo, amesema Serikali sasa inalenga hatua kubwa zaidi ya kuhakikisha ugonjwa huo unatoweka nchini.

“Ningependa twende hatua moja zaidi. Tusizungumzie tena kupunguza kipindupindu, bali tukitokomeze kabisa. Hilo linawezekana tukiamua kwa pamoja,” amesema.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za maji, vyoo bora na miundombinu ya kunawia mikono katika shule na vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, kupitia Mradi wa Uendelevu wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSST), shule za msingi 2,302 na vituo vya afya 3,764 viliwekewa miundombinu hiyo.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga Sh35.2 bilioni kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji na usafi wa mazingira katika shule 274 na vituo vya afya 274.

Amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuimarisha afya ya wananchi.

Aidha, amewaagiza wakuu wa mikoa kurejesha kampeni za usafi wa mazingira zinazofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Tamisemi, Dk Rashid Mfaume, amesema mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira pamoja na kujadili utayari wa nchi kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama Ebola, Dengue na Malaria.

Amesema pia utajadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za kitaaluma na wadau wa maendeleo katika kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mratibu wa SRWSST, Selemani Londo, amesema utekelezaji wa mikakati mbalimbali umeleta ongezeko la matumizi ya vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono katika kaya.

Amesema matumizi ya vyoo bora yameongezeka hadi asilimia 79 kutoka asilimia 77 mwaka uliopita, huku matumizi ya vifaa vya kunawia mikono yakiongezeka kutoka asilimia 42 hadi asilimia 47 kufikia Aprili 2025.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kampeni za uhamasishaji wa jamii na kuundwa kwa vikundi 1,400 vya uhamasishaji katika ngazi za jamii.

Londo amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za ucheleweshaji wa fedha za miradi kupitia maboresho ya mifumo ya usimamizi wa fedha, huku mafundi 29 wakipatiwa mafunzo maalumu ya ujenzi wa miundombinu ya afya na usafi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *