Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imemkabidhi mwanautalii na mtangazaji wa vivutio vya utalii wa Oman, Khalid Hamed Al Barwani ‘Ubalozi wa Hiyari wa Utalii wa Tanzania’.

Hatua hiyo inafuatia mafanikio makubwa ya Al Barwani kulitangaza kimataifa Shamba la Miti Sao Hill baada ya kuitembelea mwaka 2024.

Akizungumza baada ya kumkabidhi ubalozi huo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Mafuru amesema kuwa Serikali imeamua kumtambua Al Barwani kutokana na mchango wake katika kuitangaza Tanzania duniani, akieleza kuwa ubalozi huo ni sehemu ya mkakati wa kushirikisha watu mashuhuri na wadau wa kimataifa katika kuhamasisha utalii wa Tanzania.

“Mabalozi wa hiyari wa utalii ni nguzo muhimu katika kufikisha taarifa za vivutio vya Tanzania kwa masoko mapya na kuongeza ushindani wa nchi katika sekta ya utalii duniani.” Amefafanua Mafuru

Mwaka 2024 Al Barwani aliongoza kundi la watalii liitwalo Dream Team Explorers kutembelea Shamba la Miti Sao Hill ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo yanayoongoza kwa utalii wa asili na ikolojia, huku Sao Hill ikiendelea kujijengea nafasi kama kivutio kipya kinachovutia watalii wa ndani na wa kimataifa kwa misitu yake.

Uteuzi wa Al Barwani unalenga kuipa nguvu kampeni ya kuitangaza Tanzania hususani vivutio vya utalii wa misitu kama ilivyokuwa kwa Shamba la Miti Sao Hill, na kuongeza idadi ya watalii pamoja na mapato yatokanayo na sekta hiyo ambayo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni nchini.

Mhariri @moseskwindi

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *