Morogoro. Wadau wa mazingira wamependekeza hatua nne muhimu zinazopaswa kuchukuliwa, ili kunusuru maeneo oevu nchini yanayoendelea kukabiliwa na uharibifu.

Kwa mujibu wa wadau hao, ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka maeneo oevu, utoaji wa fursa mbadala za kiuchumi, utekelezaji madhubuti wa sheria na uratibu wa pamoja wa wizara za kisekta ni miongoni mwa hatua muhimu zinazopaswa kufanyiwa kazi.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa ukosefu wa elimu kuhusu uhifadhi wa maeneo oevu umechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa Bonde la Mto Kilombero, moja ya maeneo muhimu zaidi ya ikolojia nchini, lenye mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula na maji yanayoendesha uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

Kutokana na uelewa mdogo wa wananchi, shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji wa udongo wa matofali, ukataji miti na uchomaji mkaa zimeendelea kusogea hadi kwenye vyanzo vya maji. Si hivyo tu, baadhi yao hutupa taka ovyo, zikiwamo za vifungashio vya pembejeo za kilimo, ambazo huingia mtoni.

Mdau na mwanzilishi wa Shirika la Mazingira la Khanyi Foundation, Anabahati Mlay, anasema mafanikio ya uhifadhi wa maeneo oevu yatategemea kwa kiasi kikubwa namna jamii zinavyopewa elimu kuhusu umuhimu wa maeneo hayo, pamoja na kuwezeshwa kupata njia mbadala za kujipatia kipato.

“Ili kuyaokoa maeneo oevu ni lazima tushirikiane na jamii husika kwa kuwajengea uelewa wa umuhimu wake na kuwafundisha namna ya kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa tija bila kuathiri mazingira,” anasema.

Anasema, pamoja na elimu ya mazingira, wananchi wanapaswa kufundishwa shughuli mbadala za kiuchumi, ikiwamo ujasiriamali, ili kupunguza utegemezi wa shughuli zinazochangia uharibifu wa maeneo oevu na vyanzo vya maji.

Mlay anasisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa sheria za mazingira na madhara ya kuzikiuka, akieleza kuwa utekelezaji wa sheria unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa jamii.

Akitoa mfano wa shughuli zinazofanywa na shirika hilo katika eneo la Marangu, mkoani Kilimanjaro, anasema wamekuwa wakiwajengea uwezo wananchi, wakiwamo wanawake, kupanda miti ya asili huku baadhi ya serikali za vijiji na mitaa zikitenga bajeti kwa ajili ya kununua vitalu vya miti hiyo.

Vilevile, anashauri elimu ya mazingira ianze kutolewa tangu utotoni ili ijengwe kama sehemu ya utamaduni wa jamii. Pia, anasisitiza kuwa mifumo ya elimu izingatie zaidi mafunzo ya vitendo kuliko nadharia pekee.

Anasema juhudi za uhifadhi hazipaswi kutegemea miradi ya muda mfupi ya Serikali au mashirika yasiyo ya kiserikali, bali zinapaswa kuwa sehemu ya utamaduni endelevu wa jamii.

Kwa upande wake, Ofisa Miradi wa Jumuiya za Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (CWMAC), Franklin Masika, anasema ongezeko la watu wanaotafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, pamoja na uhamaji wa wafugaji, ni miongoni mwa changamoto mpya zinazozidisha shinikizo katika Bonde la Kilombero.

Anasema kati ya mwaka 2015 na 2020, Serikali ilitekeleza programu ya matumizi ya ardhi katika wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kutoa hati miliki za kimila kwa vijiji, lakini changamoto kubwa imeendelea kuwa utekelezaji na usimamizi wa mipango hiyo.

Masika anashauri kuendelea kuelimisha wananchi, kuongeza tija ya uzalishaji wa mpunga katika maeneo madogo ili kupunguza uvamizi wa maeneo oevu, pamoja na kuweka mifumo itakayowawezesha wafugaji kufuga bila kuingia kwenye vyanzo vya maji.

Mdau mwingine wa mazingira wilayani Kilombero, Said Mwendabwillah, anaonya kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, uharibifu unaoendelea katika maeneo oevu, hususan Bonde la Kilombero, unaweza kusababisha madhara makubwa ya kimazingira katika miaka ijayo.

Anasema utafiti alioufanya kwa siku 28 katika baadhi ya maeneo ya bonde hilo ulibaini kasi ya ukataji miti, kilimo kwenye vyanzo vya maji, ufugaji holela na utupaji wa taka za plastiki unaoendelea kuhatarisha mfumo wa ikolojia.

“Hali siyo nzuri. Kuna maeneo kama Iruma ambako uharibifu ni mkubwa. Watu wanakata miti hovyo, wanafuga kiholela na kufanya kilimo kwenye vyanzo vya maji. Wengi wanafanya hivyo kwa sababu ndiyo njia waliyoikuta ya kujipatia kipato au waliyoirithi kutoka kwa wazazi wao. Hivyo, wanahitaji kueleweshwa kuwa shughuli hizo zinaharibu mazingira,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, anashauri mamlaka za kisekta kuanzisha miradi mbadala ya kiuchumi kwa wananchi wanaoishi kandokando ya maeneo oevu, ikiwamo ufugaji wa nyuki na samaki kwa njia ya vizimba, sambamba na kuwapatia elimu ya uhifadhi wa mazingira.

“Ukimpa mwananchi njia mbadala ya kipato na elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa maeneo haya, uwezekano wa kuendelea kuyaharibu unapungua kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Balozi wa mazingira, Selemani Msindi, anasema pamoja na elimu kwa jamii, kuna haja ya kuwapo sera na uratibu wa pamoja kati ya wizara zinazosimamia sekta za mazingira, maji, ardhi, kilimo, mifugo na madini ili kuondoa migongano inayochangia uharibifu wa maeneo oevu.

Anasema kwa sasa si ajabu kuona taasisi moja ikichukua hatua za kulinda mazingira huku nyingine ikitoa vibali vya shughuli zinazoweza kuathiri maeneo hayo, hali inayopunguza ufanisi wa juhudi za uhifadhi.

“Kuna wakati timu za maji zinaenda kuzuia uchimbaji kwenye vyanzo vya maji, lakini zinawakuta wahusika wakiwa na vibali kutoka sekta nyingine. Hii inaonesha umuhimu wa wizara zote zinazohusika kuwa na sera na mkakati wa pamoja wa kusimamia maeneo oevu,” anasema.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, anasema usimamizi wa maeneo oevu ni jukumu la pamoja la kitaasisi na kisekta, likihusisha Wizara ya Maji, Tamisemi, sekta ya ardhi, kilimo na madini chini ya mfumo wa sheria na taratibu zilizopo.

Anasema hakuna mgongano wa kimajukumu kwa kuwa kila sekta inafanya kazi kwa mujibu wa sheria zake, huku mifumo ya uratibu na tathmini ya mazingira ikihusisha taasisi kama Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuhakikisha shughuli zote zinazingatia uendelevu wa mazingira.

Anasema miradi na shughuli za kiuchumi, kama uchimbaji wa madini au kilimo, haziwezi kuidhinishwa bila kufuata taratibu za tathmini ya mazingira na kupata vibali husika, hatua inayolenga kuhakikisha matumizi ya rasilimali hayaathiri mifumo ya asili.

Katika hatua nyingine, Msindi anasisitiza umuhimu wa kuwapatia wananchi wanaoishi karibu na maeneo oevu njia mbadala za kujikimu, ikiwamo nishati mbadala, mabirika ya kunyweshea mifugo, maeneo mbadala ya kilimo na skimu za umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa moja kwa moja kwenye vyanzo vya maji na misitu.

Anasema utekelezaji wa sheria za mazingira unapaswa kufanywa bila kuingiliwa na masilahi ya kisiasa, akieleza kuwa wakati mwingine viongozi husita kuchukua hatua dhidi ya waharibifu wa mazingira kwa hofu ya kupoteza uungwaji mkono wa kisiasa.

“Sheria zipo, lakini ni lazima zitekelezwe bila kuingizwa siasa. Vilevile, kampeni za uhifadhi zielekezwe zaidi kwenye maeneo halisi ya vyanzo vya maji badala ya kujikita mijini pekee, ambako athari za uharibifu zinaanzia mbali na wananchi wanaohusika moja kwa moja,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *