Mahakama ya Zanzibar imeendelea kuboresha utoaji wa huduma zake kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa haki. Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (Electronic Case Management System–eCMS), ulioanza kutumika rasmi katika Mahakama za Kawaida na Mahakama za Kadhi kuanzia Julai 1, 2026.

Mfumo huo utasimamia hatua zote za mashauri, kuanzia ufunguaji wa kesi, usajili, usikilizaji hadi utoaji wa hukumu. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, utekelezaji wake utafanyika kwa awamu tatu ili kuhakikisha mabadiliko kutoka mfumo wa analojia kwenda kidijitali yanafanyika kwa ufanisi.

Awamu ya kwanza imeanza Julai 1, 2026 ikihusisha Mahakama Kuu Masjala Kuu Tunguu na Divisheni zake, Mahakama ya Kadhi wa Rufaa Tunguu pamoja na Mahakama zote za Mkoa wa Mjini Magharibi. Awamu ya pili itaanza Agosti 1, 2026 katika Mahakama zote za Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kusini Unguja, huku awamu ya tatu ikianza Septemba 1, 2026 ikihusisha Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Pemba, Mahakama ya Kadhi wa Rufaa Pemba pamoja na Mahakama zote za Kaskazini na Kusini Pemba.

Kwa mujibu wa Mahakama, mashauri yatakayofunguliwa katika kipindi hicho yatakuwa mashauri mapya pekee. Mashauri yote yaliyofunguliwa kabla ya Julai 1, 2026 yataendelea kusikilizwa kwa utaratibu wa zamani. Aidha, katika usikilizaji wa awali wa mashauri ya jinai, kumbukumbu zitachapishwa, kusainiwa na wahusika kabla ya kuskaniwa na kuhifadhiwa kwenye mfumo wa eCMS. Vivyo hivyo, rufaa na maombi yanayotokana na mashauri yaliyoanza kwa mfumo wa zamani yataendelea kuendeshwa kwa utaratibu huo, huku kumbukumbu zote zitakazohifadhiwa kwenye eCMS zikitambuliwa kuwa kumbukumbu rasmi za Mahakama.

Kutokana na mfumo huo kuwa mpya, kutakuwa na madawati ya usaidizi katika kila Mahakama kwa ajili ya kuwasaidia wananchi watakaohitaji msaada wa matumizi ya mfumo. Pia, mara mfumo utakapoanza kutumika katika Mahakama husika, hakutakuwa na mashauri mapya yatakayopokelewa kwa mfumo wa zamani isipokuwa kwa maelekezo ya Jaji Mkuu. Mwongozo huo unaweza pia kufanyiwa marekebisho kadiri mahitaji yatakavyojitokeza.

Hatua hii inastahili pongezi. Mahakama ya Zanzibar imeonyesha utayari wa kwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali yanayoendelea duniani. Leo karibu kila sekta inategemea teknolojia ili kuongeza ufanisi na kuboresha huduma, hivyo ni muhimu taasisi ya utoaji haki nayo isibaki nyuma.

Hata hivyo, mafanikio ya mfumo huu hayatategemea uzinduzi wake pekee, bali uwezo wake wa kufanya kazi kwa ufanisi. Tumeshuhudia katika taasisi mbalimbali mifumo ya kidijitali ikikwama mara kwa mara kutokana na hitilafu za kiufundi, mtandao kukatika au mfumo kushindwa kufanya kazi kwa wakati. Hali kama hiyo huleta usumbufu kwa wananchi na kupunguza imani kwa huduma zinazotolewa.

Lengo la matumizi ya teknolojia ni kurahisisha huduma, kupunguza muda na kuondoa urasimu. Hivyo, ni muhimu Mahakama ihakikishe mfumo wa eCMS unakuwa imara, salama na wenye matengenezo ya wakati ili usiwe chanzo cha changamoto mpya badala ya kuwa suluhisho.

Vilevile, elimu kwa wananchi ni jambo lisilopaswa kupuuzwa. Mfumo unaweza kuwa bora, lakini usipofahamika kwa watumiaji wake hautafikia malengo yaliyokusudiwa. Mahakama inapaswa kuendelea kutoa elimu ya kutosha ili wananchi wauelewe na kuutumia kwa ufanisi.

Aidha, madawati ya usaidizi yanapaswa kusimamiwa kwa karibu ili yasitoe mwanya kwa watu wasiokuwa waaminifu kujinufaisha kwa kuwatoza wananchi fedha kinyume cha utaratibu kwa kisingizio cha kuwasaidia kutumia mfumo. Uzoefu unaonyesha mazingira ya utoaji huduma wakati mwingine huvutia watu wa aina hiyo, hivyo usimamizi madhubuti unahitajika.

Iwapo mfumo huu utasimamiwa vizuri, utapunguza gharama zisizo za lazima, kuokoa muda wa wananchi na kuongeza kasi ya utoaji wa haki. Vilevile, utarahisisha utendaji wa majaji na mahakimu kwa kutumia teknolojia pale sheria na taratibu zinaporuhusu.

Kwa ujumla, kuanza kutumika kwa mfumo wa eCMS ni hatua muhimu katika safari ya Mahakama ya Zanzibar ya kuboresha utoaji wa haki. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kwa ufanisi, wananchi wanapatiwa elimu ya kutosha na changamoto zinazoweza kujitokeza zinatatuliwa kwa wakati. Hapo ndipo lengo la kutumia teknolojia katika utoaji wa haki litakapokuwa limefikiwa kwa manufaa ya wananchi wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *