Chanzo cha picha, Reuters
Marekani imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, huku milipuko ikiripotiwa katika maeneo ya kusini mwa nchi, ikiwemo karibu na Bandar Abbas na maeneo mengine ya pwani.
Maafisa wa Marekani wamesema mashambulizi hayo yanalenga kupunguza uwezo wa Iran wa kutishia usafiri wa majini katika Mlango bahari wa Hormuz, kufuatia mashambulizi yaliyodaiwa kufanywa na Iran dhidi ya meli za kibiashara.
Iran imekosoa mashambulizi hayo na kuyataja kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku ikidai kujibu kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba.
Mvutano huo umeongeza hofu ya kuenea kwa mzozo katika Mashariki ya Kati na kusababisha bei za mafuta kupanda katika masoko ya dunia.
Milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Iran, ikiwemo miji ya Konarak na Chabahar.
Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa milipuko minane imetokea katika mji wa Bandar Abbas, huku ikidai kwamba makombora mawili yalipiga bandari za Sirik na Jask, ambazo zote ziko kusini mwa Iran.
Vyombo vya habari vya serikali pia vilisema kuwa makombora mawili yalilipiga kisiwa cha Abu Musa, eneo ambalo limekuwa likizozaniwa umiliki kwa muda mrefu kati ya Iran na Falme za Kiarabu.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya serikali ya Iran, mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa katika mji wa Bandar Abbas kufuatia mashambulizi hayo.
Kiwango halisi cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Marekani bado hakijajulikana. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kukatika kwa umeme katika mji wa Chabahar na kuzuka kwa moto katika kambi ya Jeshi la Iran mjini Bushehr.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One, Jumatano jioni, Rais Donald Trump alisema Iran ilikuwa imewasiliana na Marekani muda mfupi uliopita na ilikuwa “inataka kufikia makubaliano kwa udi na uvumba.”
Trump aliongeza: “Sijui kama wanafaa kufanya makubaliano. Sijui kama watayaheshimu makubaliano hayo, hilo ndilo tatizo.”
Unaweza kusoma;