Dar es Salaam. Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimetoa mapendekezo manane kikitaka maboresho ya sheria na utaratibu wa kushughulikia wanataaluma.

Kimesema kukamatwa kwa wahadhiri kwa tuhuma zinazohusiana na shughuli zao kunaleta athari kwa elimu ya juu, utafiti na maendeleo ya demokrasia nchini.

Mapendekezo hayo yanakuja kufuatia kukamatwa kwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage kwa madai ya kuhamasisha maandamano ya Julai 7, 2026.

Tukio la kukamatwa kwa Kaijange limedhibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera leo Jumatatu, Julai 20, 2026, baada ya Mwananchi kumtafuta kuzungumzia tukio hilo akisema ni kweli wanamshikilia Kaijage.

”Ni kweli tunamshikilia kwa tuhuma hizo, lakini maelezo zaidi kwa sasa tuache maana tuko kwenye uchunguzi zaidi kwa mtuhumiwa na uchunguzi ukikamilika kila kitu kitawekwa wazi ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vingine vya sheria,” amesema

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa THTU, Dk Paul Loisulie wahadhiri wengine wawili wa Chuo Kikuu cha St. John Tanzania (SJUT) walikamatwa kwa tuhuma kama hizo za kuhamasisha maandamano ya Julai 7, 2026.

Dk Loisulie amesema wahadhiri hao wamekamatwa kwenye mazingira yanayoibua maswali kuhusu uhuru wa taaluma na utekelezaji wa sheria.

Dk Loisulie amesema mmoja wa wahadhiri wa SJUT amekamatwa baada ya kufundisha mada ya maadili na utawala bora, akitumia mifano ya kashfa zilizowahi kutokea nchini ikiwemo Richmond, Escrow na nyingine na namna wanasiasa walivyowajibika kwa kutozingatia taratibu.

Dk Loisulie ametaja lengo la mifano hiyo kutumika kulingana na wahusika wenyewe, ni kuwaelewesha wanafunzi umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu wanapotekeleza majukumu yao baadaye watakapokuwa kazini.

Mhadhiri mwingine ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi alihusishwa na masuala ya uchaguzi wa wanafunzi chuoni.

“Wote wawili walikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano ya Julai 7,2026,”amesema Dk Loisulie kupitia taarifa yake hiyo yenye kurasa 14.

Tukio lingine ni la Kaijage ambaye alikamatwa baada ya kuitikia wito wa Jeshi la Polisi iliyomtaka afike kituo kimojawapo cha Polisi kwa tuhuma hizohizo za kuhamasisha maandamano.

“Bahati mbaya zaidi, huyu wa UDOM ni mara ya pili anakamatwa, mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana kwenye vuguvugu la maandamano ya Desemba 9, 2025,” ameandika Dk Loisulie.

Kufuatia tukio hilo, Mwenyekiti wa Umoja wa wanataaluma chuo kikuu cha Dodoma (Udomasa), Dk Gerald Shija amesema wanaendelea kupambania haki ya Mhadhiri huyo ili kujua ukweli kama ni kisa cha kuhamasisha maandamano au kutakuwa na jambo lingine nyuma ya pazia.

Mapendekezo ya THTU

Kufuatia tukio hilo, THTU imependekeza Serikali kufanya marekebisho ya sheria ya vyuo vikuu ili kutambua wazi uhuru wa taaluma kama haki ya msingi katika elimu ya juu.

“Sheria ya Vyuo Vikuu Na. 7 ya mwaka 2005 inapaswa kufanyiwa marekebisho ili kujumuisha masharti yanayolinda uhuru wa kufundisha, kufanya utafiti, kuchapisha matokeo ya tafiti na kushiriki katika mijadala ya kitaaluma bila kuingiliwa isivyo halali,” amesema Dk Loisulie.

Mapendekezo mengine, ni vyombo vya dola kutofautisha shughuli halali za kitaaluma na makosa ya jinai, huku vyuo vikuu vikitakiwa kuimarisha uhuru wa taasisi kwa kuweka sera zinazolinda uhuru wa wanataaluma.

Pia kimependekeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), vyama vya wafanyakazi na jumuiya za wanataaluma kushirikiana kuandaa miongozo ya kitaifa kuhusu uhuru wa taaluma.

Pendekezo la mwisho ni Tanzania kuendelea kutekeleza viwango vya kimataifa vinavyolinda uhuru wa taaluma, ikiwemo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Mapendekezo ya Unesco ya mwaka 1997), Azimio la Dar es Salaam la mwaka 1990 na Azimio la Kampala la mwaka 1990.

Mwananchi ilifanya jitihada za   kuipata Serikali kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia juu ya mapendekezo hayo bila mafanikio.

Athari kuingilia taaluma

Mbali na mapendekezo hayo, THTU imesema ukamataji wa wahadhiri wanapotekeleza majukumu yao kunaleta athari kwa mtu binafsi, familia, Serikali na sekta ya elimu ya juu.

“Athari hizo ni pamoja na kuzalisha hofu miongoni mwa wanataaluma, hali inayowafanya wahadhiri na watafiti kujizuia kufundisha au kufanya tafiti kuhusu masuala yanayoonekana kuwa nyeti,”amesema.

Lingine ni kushusha ubora wa ufundishaji kutokana na wahadhiri kuepuka mijadala ya kisiasa, kijamii na kikatiba, jambo litakalowanyima wanafunzi uwezo wa kujenga fikra pevu na kuchambua hoja, kudhoofika kwa tafiti na uchapishaji wa kazi za kisayansi, kupungua kwa uhuru wa taasisi za elimu ya juu kujiendesha. Pia kuathirika kwa uhusiano kati ya walimu na wanafunzi na kupungua kwa ushiriki wa wanafunzi kwenye mijadala ya kitaaluma.

“Mazingira hayo yanaathiri taswira ya vyuo vikuu vya Tanzania kimataifa na kupunguza fursa za ushirikiano wa kitaaluma, ufadhili wa tafiti na ubadilishanaji wa wataalamu,”amesema Dk Loisulie.

THTU, imeeleza athari hizo zinaweza pia kudhoofisha mchango wa wanataaluma katika mijadala ya sera za umma, hivyo kuathiri maendeleo ya demokrasia, utawala bora na mfumo mzima wa elimu ya juu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *