
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limethibitisha kufanya mashambulio dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait na Jordan, likisisitiza kuwa kulenga kambi zinazotumiwa katika operesheni dhidi ya Iran ni “haki ya Iran ya kisheria, kidini, na kimantiki.”
Katika taarifa mbili tofauti zilizoelekezwa kwa wananchi wa Kuwait na Jordan, IRGC imebainisha kuwa operesheni hizo zilifanyika ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya uchokozi wa mara kwa mara wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
IRGC imebainisha kuwa vikosi vyake vilishambulia Kambi ya Anga ya Ali Al Salem nchini Kuwait, na kufanikiwa kuharibu mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot, ghala kubwa la vifaa vya kijeshi, pamoja na maegesho ya ndege zisizo na rubani aina ya MQ-9. Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa mashambulio ya ndege zisizo na rubani yalilenga kambi ya wanajeshi wa Marekani na maegesho ya helikopta katika Kambi ya Udairi, na kusababisha majeruhi na uharibifu mkubwa wa helikopta na ndege hizo zisizo na rubani.
Nchini Jordan, IRGC imetangaza kuharibu rada ya mfumo wa ulinzi wa makombora wa THAAD, mfumo wa Patriot, na rada ya C-RAM katika kambi ya Marekani. Mashambulio hayo ya usahihi wa hali ya juu yamesababisha milipuko ya moto katika vituo vya kuhifadhia mafuta, ghala la vifaa vya helikopta, na hangar ya matengenezo ya helikopta.
Katika taarifa zake, IRGC imekanusha vikali madai ya “uwongo mtupu” kwamba mashambulio yake dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani yanakiuka uhuru, mamlaka ya ardhi, na utimilifu wa nchi za ukanda huo.
IRGC imesisitiza: “Kwa mtazamo wetu, uhuru, mamlaka ya ardhi, na utimilifu wa serikali yenu unaheshimiwa kikamilifu.”
Jeshi hilo liliongeza kuwa kambi za kijeshi za Marekani zinafanya kazi chini ya mamlaka ya Marekani badala ya mamlaka ya wenyeji, ikibainisha kuwa vituo hivyo vinadhibitiwa na Wamarekani bila kuingiliwa na mamlaka za nchi za ukanda huo.
IRGC ilihitimisha kwa kusema: “Marekani ndiyo inayokiuka mamlaka yenu ya ardhi na si Iran.” Jeshi hilo lilisisitiza, “Iran inashambulia ardhi inayokaliwa na jeshi la Marekani, jeshi lisilojua kitu kingine isipokuwa uhalifu.”
Taarifa hiyo pia imekumbushia tukio la kuzikwa kwa mabaki ya wanafunzi waliouawa shahidi katika shambulio la anga la Marekani kwenye shule ya msingi ya Iran katika mji wa kusini wa Minab, katika siku ya kwanza ya uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni mnamo tarehe 28 Februari.
IRGC imesema:“Jana, wananchi wenye majonzi wa Minab walifanya mazishi kwa ajili ya mabaki ya watoto wao wa shule, ambayo yaligunduliwa chini ya vifusi, na kuwazika katika nyumba zao za milele.”
IRGC imebainisha kuwa watu 168, wengi wao wakiwa wanafunzi, waliuawa katika siku ya kwanza ya vita hivyo katika shambulio lililofanywa na “jeshi la Marekani linaloua watoto”. Taarifa hiyo imebaini kuwa uhalifu huo unaendelea huku baadhi ukitekelezwa kwa kutumia kambi za Marekani katika eneo.
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limesisitiza: “Ni haki yetu ya kisheria, kidini, na kimantiki kuwalenga wavamizi wa nchi yetu na wauaji wa watoto wetu pale wanapotushambulia.”