Idadi ya vifo kutokana na mlipuko wa sasa wa virusi vya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imefikia watu zaidi ya 1,000.

Hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na mamlaka za afya nchini humo huku maambukizi mapya yakizidi kuongezeka.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikiripoti ongezeko mtawalia la maambukizi mapya tangu mlipuko huo utangazwe tarehe 15 Mei mwaka huu.

Takwimu za Wizara ya Afya zimeonyesha kuwa watu 2,536 wameambukizwa Ebola hadi sasa nchini Kongo tangu kutangazwa mlipuko wa ugonjwa huo mwezi Mei mwaka huu.

Watu 1,033 wamethibitishwa kupoteza maisha kutokana na Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hii ni katika hali ambayo wagonjwa 738 kwa sasa wako katika karantini au wamelazwa hospitalini, huku watu wengine 506 wakithibitika kupona Ebola.

Wiki iliyopita, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji lilionya kuwa usafirishaji wa miili ya wahanga wa Ebola kote nchini Kongo kwa ajili ya kuzikwa katika jamii zao za asili unazidisha hatari ya virusi hivyo kuendelea kusambaa.

Virusi hivyo vimeathiri majimbo matano, yakiwemo Haut-Uele, Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tshopo.

Ituri inaendelea kuwa kitovu cha mlipuko unaosababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo, huku maambukizi yakiendelea bila kusita.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuenea kwa kasi ya kutisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ameonya kuwa iwapo mataifa mbalimbali hayatachukua hatua madhubuti za kuzuia maambukizi ya virusi hivyo, “mlipuko wa sasa utageuka kuwa mbaya zaidi ambao dunia imewahi kushuhudia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *