Tanga. Mvutano kuhusu matumizi ya Stendi kuu ya mabasi Kange umeingia katika hatua mpya baada ya kamati ya fedha na uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kupendekeza kituo hicho kibadilishwe matumizi na kuwa maegesho ya malori iwapo mpango wa kuhamishia mabasi utaendelea kukwama.
Mapendekezo hayo yametolewa leo Alhamisi, Julai 23, 2026, baada ya kamati hiyo kutembelea stendi hiyo na kujadili hatima yake kufuatia kusuasua kwa utekelezaji wa uamuzi wa kuhamishia huduma za mabasi katika eneo hilo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Meya wa Jiji la Tanga na Mwenyekiti wa kamati ya fedha na uongozi, Mustapha Muhina, maarufu Seleboss, amesema kamati imesikitishwa na kusimamishwa kwa jitihada za Halmashauri kuanza kutumia stendi hiyo licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.
Amesema halmashauri ilikuwa ikitekeleza maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu–Tamisemi yaliyozitaka halmashauri kutumia vituo vikuu vya mabasi kwa mujibu wa sheria, lakini baadaye ikaelekezwa kusitisha utekelezaji na kuruhusu mabasi kuendelea kupakia na kushusha abiria katikati ya jiji.
“Tumewekeza fedha nyingi kujenga kituo hiki kwa lengo la kuongeza mapato ya Jiji na kupunguza msongamano. Hatuwezi kuendelea kukiacha bila matumizi wakati mabasi yanaendelea kufanya shughuli zake mjini,” amesema.
Muhina amesema kamati imeazimia kuwasilisha pendekezo hilo katika baraza la madiwani ili stendi hiyo ibadilishwe kuwa maegesho ya malori endapo juhudi za kuhamishia mabasi zitashindikana. Amesema hatua hiyo italinda uwekezaji wa Serikali na kuhakikisha kituo hicho kinachangia mapato ya halmashauri.
Ameeleza kuwa halmashauri ilisimamisha utekelezaji wa mpango huo baada ya ushauri wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), lakini baadaye ilipokea barua ya Tamisemi ya Juni 12, 2026 iliyosisitiza vituo vikuu vya mabasi vitumike kama ilivyokusudiwa. Hata hivyo, halmashauri iliweka utaratibu wa mpito ulioruhusu mabasi ya alfajiri kuondoka katika ofisi zao huku safari za mchana zikianzia Kange.
Shughuli za usafirishaji zikiendelea katika kituo kikuu cha Kange zikiendelea huku kukiwa na shinikizo kubwa la magari yote kuanzia safari hapo badala ya kuanzia katikati ya jiji la kupitia humo. Picha na Mbonea Herman
Diwani wa Kata ya Maweni na mjumbe wa kamati ya fedha na uongozi, Joseph Colyvas, amesema anaunga mkono kubadili matumizi ya stendi hiyo iwapo itaendelea kushindwa kutumika. Amesema kituo hicho kilijengwa kwa gharama kubwa hivyo hakipaswi kubaki bila matumizi.
“Kama mabasi hayawezi kutumia kituo hicho, ni bora kibadilishwe matumizi kuliko kuendelea kuwa uwekezaji usiozalisha tija,” amesema. Ameongeza kuwa hoja ya umbali wa Kange haipaswi kuzuia matumizi yake kwa kuwa wasafiri kutoka Lushoto na Handeni tayari wanakitumia.
Kwa upande wao, waendeshaji wa mabasi kupitia Umoja wa Wasafirishaji Mkoa wa Tanga (Taboa), wamesema hawapingi matumizi ya stendi ya Kange bali wanataka makubaliano ya awali yaheshimiwe. Makamu Mwenyekiti wa Taboa Mkoa wa Tanga, Albert Peter, amesema walikubaliana kwanza kuboresha huduma muhimu ikiwamo viti vya abiria, kituo cha polisi, zahanati, maeneo ya chakula na maegesho ya daladala. “Hatupingi Kange. Tunataka mazingira yawe tayari kwanza kwa sababu bado hakuna baadhi ya huduma muhimu tulizokubaliana nazo,” amesema.
Albert amesema Taboa imependekeza mabasi yaendelee kupakia abiria katika ofisi zao huku yakipitia Kange kulipa ushuru wa Sh5,000 kwa siku hadi miundombinu yote itakapokamilika.
Mvutano huo umeendelea kwa miezi kadhaa kutokana na tofauti za msimamo kati ya baraza la madiwani na RCC. Wakati Baraza lilipitisha azimio la mabasi yote kuhamia Kange kuanzia Julai 1 mwaka huu, RCC ilishauri utekelezaji usitishwe kwa muda kutokana na changamoto za usafiri, usalama na ukosefu wa baadhi ya huduma muhimu.