Unguja. Zanzibar imezindua rasmi huduma ya usafiri wa umma kwa kutumia mabasi ya umeme, ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa usafiri wa kisasa, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri kwa wananchi.
Akizindua huduma hiyo, leo Julai 23, 2026 Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha visiwa hivyo vinahamia kikamilifu katika matumizi ya magari ya umeme.
Amesema mpango huo utahusisha magari ya usafiri wa umma, magari ya Serikali na baadaye magari binafsi, kwa lengo la kujenga miji safi, rafiki kwa mazingira na inayokwenda sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kushirikiana na kampuni ya GRT kutoka India.
Unatarajiwa kuwa na jumla ya mabasi 500, na katika awamu ya kwanza mabasi 15 yameanza kutoa huduma, huku mengine yakisubiri kukamilika kwa miundombinu inayojengwa katika maeneo mbalimbali.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwa kwenye moja ya mabasi ya umeme katika hafla ya uzinduzi wa mabasi hayo katika Kituo cha mabasi Malindi Unguja Zanzibar
Tofauti na mfumo wa kawaida wa usafiri wa umma, abiria watatumia kadi maalumu kulipia nauli.
Kadi hizo zimegawanywa katika makundi matatu: kadi ya rangi ya buluu kwa abiria wa kawaida watakaolipa Sh700, kadi ya rangi ya dhahabu kwa wanafunzi, na kadi ya rangi nyeusi kwa wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, ambao watalipa nusu ya nauli, sawa na Sh350.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabasi hayo ulioambatana na ufunguzi wa kituo cha mabasi cha Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Dk Mwinyi amesema uzinduzi huo ni mwanzo wa mpango mpana wa kuhamia matumizi ya magari ya umeme Zanzibar.
“Tumeanza na mabasi haya 15, lakini tutakuwa na mabasi 500. Tukikamilisha usafiri wa umma, tutahamia kwenye magari ya Serikali ili nayo yatumie umeme, na baadaye tutahamasisha magari ya watu binafsi. Tunataka Zanzibar nzima itumie magari ya umeme pekee,” amesema.
Ameitaka ZSSF kuhakikisha ujenzi wa vituo vyote vya mabasi unakamilika kwa wakati ili mradi huo uanze kutoa huduma kamili kwa wananchi na wageni.
Sehemu ya mabasi ya umeme yaliyozinduliwa kuanza kutoa huduma yakiwa yameegeshwa katika kituo cha mabasi Malindi
“Napenda nitoe wito kwa ZSSF kuhakikisha vituo vyote vya mabasi vinavyoendelea kujengwa vinakamilika haraka, ili mradi huu ukamilike kwa wakati na wananchi pamoja na wageni wanufaike na huduma hii,” amesema.
Rais Mwinyi amesema pia mfumo huo utasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili wanafunzi wanapotumia usafiri wa umma, akieleza kuwa watapata mazingira salama na yenye heshima bila kubaguliwa au kunyanyaswa kwa sababu ya kulipa nauli ya punguzo.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF, Nassor Shaaban Ameir, amesema hatua inayofuata baada ya kuwasili kwa mabasi hayo ni ujenzi wa vituo vya mabasi katika maeneo ya Mwera, Jumbi na Mnazi Mmoja ili kurahisisha utoaji wa huduma za usafiri kwa wananchi.
Amesema mabasi mengine 35 yamekamilika kutengenezwa na yanasubiri kukamilika kwa miundombinu pamoja na njia maalumu za usafiri kabla ya kuanza kutoa huduma rasmi.
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua ya kuanzishwa kwa mfumo huo wa usafiri wa kisasa, wakieleza matumaini kwamba utaleta ahueni ya changamoto za usafiri wa umma na kuboresha huduma kwa wasafiri. Hata hivyo, wengine wameeleza wasiwasi kuhusu namna watakavyotumia kadi za kielektroniki kulipia nauli.
Khadija Saleh Haji, mkazi wa Kiembesamaki, amesema ujio wa mabasi hayo ni maendeleo makubwa kwa Zanzibar.
“Ni jambo la kheri kuwa na usafiri mzuri. Tulikuwa tukiuona kwa wenzetu katika nchi nyingine, lakini leo na sisi tumepata mabasi ya kisasa na yenye ubora. Tunaamini yatasaidia kurahisisha usafiri na kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema.
Mashindano ya AFCON
Akizungumza kuhusu madai kwamba Serikali imetumia zaidi ya Sh1.4 trilioni kujenga uwanja wa AFCON na fedha hizo haziwezi kurudi, Dk Mwinyi amekanusha, akisema kwanza hiyo si gharama halisi, badala yake zinatumika Dola milioni 150 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh300 bilioni.
Licha ya kutomtaja, kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa ACT, Othman Masoud, katika mahojiano maalumu na chombo kimoja cha habari hapa nchini.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akipokea moja ya mfanano wa kadi zitakazokuwa zikitumiwa na abiria kupanda mabasi ya umeme baada ya kuzindua safari zake katika kituo cha mabasi Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi
Hata hivyo, amesema kuwapo kwa AFCON ni hatua ya kukuza utalii wa michezo, kwani kuna uwanja wa mpira, viwanja vidogo vya mazoezi, bwawa la kuogelea la ukubwa wa viwango vya Olimpiki, pamoja na miradi kadhaa pembeni yake.
“Lakini tunajenga mji, hatujengi uwanja wa mpira. Pembeni kutakuwa na nyumba za makazi, hoteli na kumbi za mikutano. Ule utabadilika kuwa mji wa maendeleo wa kisasa. Sasa, kama mtu hajui faida ya hayo, nataka nimueleze: faida ya michezo, huu tunaita utalii wa michezo, idadi ya watu watakaokuja Zanzibar itaongezeka,” amesema.