Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6
Marekani ilitangaza Jumatano Julai 22 kwamba imefikia makubaliano ya nyuklia ambayo haijawahi kushuhudiwa na Saudi Arabia ambayo itaiwezesha nchi hiyo ya Mashariki ya Kati kuendeleza sekta yake ya nishati.
Waziri wa Nishati wa Marekani na mwenzake wa Saudi Arabia Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman walitia saini “Makubaliano ya 123” kuhusu ushirikiano wa nyuklia “kwa madhumuni ya amani,” pamoja na makubaliano ya pande mbili yanayoambatana nayo kuhusu hatua za uangalizi na udhibiti, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.
“Kwa pamoja, makubaliano haya mawili yanaweka msingi wa kisheria wa ushirikiano wa miongo kadhaa na wenye thamani ya mabilioni ya dola, ambao unachochea malengo kadhaa muhimu ya kiuchumi na kimkakati, ikiwemo kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia,” taarifa ilisema.
Makubaliano hayo yameibua hofu kwamba yanaweza kuchochea mbio za utengenezaji wa silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo tayari linakabiliwa na hali hali tete ya kiusalama.
Waziri Wright alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari: “Msiwe na shaka makubaliano haya yanazingatia viwango vya juu zaidi vya usalama wa nyuklia na kuzuia kuenea kwa silaha hizo, na yameegemezwa kwenye teknolojia bora zaidi ya nyuklia na wanasayansi mahiri duniani, yote yamebuniwa hapa Marekani.”
Makubaliano hayo yatawasilishwa katika Bunge la Marekani kwa alijili ya kufanyiwa tathmini.
Kwa mujibu wa ripoti ya awali ya CBS News—mtandao wa habari wa Marekani unaoshirikiana na BBC—lengo mojawapo la makubaliano hayo ni makampuni ya Marekani kusimamia mitambo ya kuzalisha nishati ya nyuklia ndani ya ardhi ya Saudi Arabia.
Makampuni yanayohusika na mpango huo bado hayajatangazwa rasmi. Kwa mujibu wa CBS, mojawapo ya makampuni hayo ni Westinghouse Electric Company.
Saudi Arabia kwa sasa haina mitambo yoyote ya kuzalisha nishati ya nyuklia, lakini mnamo Septemba 2023, Waziri wake wa Kawi alisisitiza tena nia ya nchi hiyo kujenga mtambo wa aina hiyo.
Kulingana na takwimu za hivi punde kuhusu Saudi Arabia kutoka kwa Shirika la Habari za Nishati la Marekani (EIA), vyanzo vya nishati vya nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ni gesi asilia (asilimia 62), mafuta (asilimia 38), na nishati mbadala inayochukua chini ya asilimia moja.
Rosemary Kelanic, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, anasema kuwa uwezekano wa Marekani kuruhusu urutubishaji wa urani ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ni jambo la “kushangaza sana.”
“Marekani haijawahi kufanya jambo kama hili hapo awali; hatujawahi kusaidia nchi nyingine kurutubisha urani ndani ya ardhi yake,” aliambia BBC.
Kulingana na Kelanic, sababu ni kwamba “ikiwa unaweza kuzalisha mafuta yako mwenyewe ya nyuklia, unakuwa na hatari kubwa zaidi” kuhusiana na utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Chanzo cha picha, Getty Images
Maoni tofauti
Tangazo la makubaliano hayo asubuhi ya Jumatano, lilizua maoni mbalimbali nchini Marekani na kote duniani.
Nchini Israel, Waziri wa Uchumi Nir Barkat alisema nchi yake haipingi Saudi Arabia kumiliki nishati ya nyuklia ili mradi tu isitumike nje ya muktadha wa uzalishaji nishati.
“Iwapo wanaitaka kwa ajili ya matumizi ya amani, tunaweza kulikubali hilo. Wamarekani hawataki kuiweka Israel hatarini. [Waziri Mkuu] Netanyahu na Trump wanajua jinsi ya kushughulikia mambo kwa umakini,” Barkat aliambia kituo cha redio cha jeshi la Israel.
Hata hivyo, kwa mtazamo wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Israel, Avigdor Liberman, nchi yake inapaswa kuzuia makubaliano hayo.
“Mpango wa nyuklia wa kiraia wa Saudi Arabia hatimaye utaishia kwenye silaha za nyuklia,” aliandika kwenye mtandao wa X, akiongeza kuwa hatua hiyo ingesababisha “mbio za kumiliki silaha katika eneo la Mashariki ya Kati.”
Chanzo cha picha, Reuters
Mjini Washington, Brad Sherman, mbunge wa chama cha Democratic kutoka California, alisema kuwa Marekani inapaswa kuidhinisha makubaliano ya aina hiyo ikiwa tu yatakuwa na “dhamana ya kiwango cha juu” kama zile zilizopo katika makubaliano yao na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Chini ya makubaliano hayo ya mwaka 2009, UAE hazizalishi urani yake yenyewe.
“Rais aliye vitani ili kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati hapaswi kuwezesha mpango kama huo kwa sababu makampuni ya Marekani yanatarajia kupata faida,” Sherman aliandika kwenye mtandao wa X.
Mbunge mwenzake wa chama cha Democratic, John Garamendi, alielezea makubaliano hayo kama “sera mbaya sana” ambayo haipaswi “kamwe” kuruhusiwa.
“Urani iliyorutubishwa inaweza kutumika kutengeneza silaha ya nyuklia. Hii ni sera mbaya sana,” aliambia CNN.
Mbunge wa chama cha Republican, Marlin Stutzman, aliambia chombo hicho hicho cha habari kuwa hana “mashaka” kuhusu makubaliano hayo, lakini angependa “kupata taarifa zaidi kutoka kwa vyombo vya usalama na ujasusi.”
“Kwa kweli, Saudi Arabia ndiyo nguzo ya utulivu katika Mashariki ya Kati,” alisema.
Chanzo cha picha, Getty Images
Je, kuna msingi wowote wa hofu kwamba Saudi Arabia huenda ikajaribu kutengeneza silaha za nyuklia?
Na Frank Gardner, Mwandishi wa BBC wa Masuala ya Usalama
Je, Saudia itataka kuwa na bomu la nyuklia?
Hapana. Walau kwa mambo yalivyo leo. Lakini hiyo ndiyo hofu ambayo bila shaka inazingira makubaliano haya.
Iran ilirutubisha urani yake na tunaweza kuona kilichotokea huko.
Ndani ya milima yake ya jangwani, nje ya uwezo wa satelaiti za Marekani, Jamhuri ya Kiislamu iliendelea mbele na kurutubisha kilo 441 za urani hadi ikafikia asilimia 60, zaidi ya asilimia 3.67 inayohitajika kwa nishati ya nyuklia ya matumizi ya kiraia na hatua moja tu kutoka kwa urani iliyorutubishwa sana ya kijeshi (HEU) inayohitajika kutengeneza bomu.
Inaaminika kuwa urani hii iliyorutubishwa sana imesalia kwenye vichuguu vilivyolipuliwa mwaka jana wakati wa operesheni ya Marekani ya “Midnight Hammer”.
Hakuna chochote kinachoonyesha kuwa Saudi Arabia ina nia yoyote ya kufuata nyayo za Iran, au kuelekeza mpango wake changa wa nyuklia wa kiraia kwa masla malengo ya kijeshi.
Lakini Wasaudia wanaishi katika eneo hatari, na ikiwa Iran ingepata silaha ya nyuklia, wangetaka kuwa nayo kama kizuizi.
Lakini, badala ya kupitia mchakato mrefu, mgumu, na haramu wa kurutubisha urani yao hadi 90% na kisha kuigeuza kuwa kichwa cha nyuklia, kidharia wangeweza kununua bomu ambalo liko “tayari kutumia” kutoka kwa mshirika wao Pakistan.
Mashauriano ya miaka mingi
Mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nishati ya nyuklia kati ya Marekani na Saudi Arabia yalianza mwaka wa 2008.
Wakati wa utawala wa George W. Bush, nchi hizo mbili zilitia saini mkataba wa maelewano, ambapo Washington iliahidi kuisaidia Riyadh kuendeleza nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.
Saudi Arabia ilikuwa imesema inakusudia kuagiza mafuta ya nyuklia na haitatafuta “teknolojia nyeti za nyuklia”.
Hizi ni baadhi ya hatua muhimu zilizofikiwa tangu wakati huo:
- Kati ya mwaka wa 2017 na 2019, Marekani ilizipa kampuni saba za Marekani idhini ya kufanya “mazungumzo kuhusu nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia” na Saudi Arabia.
- Mwaka wa 2020, Ofisi ya Uwajibikaji wa Serikali ya Marekani (GAO) iliripoti kuwa nchi hizo mbili “hazikuwa zimepiga hatua kubwa” kutokana na “tofauti zinazoendelea” kuhusu masuala kama vile vikwazo vya urutubishaji.
- Mwaka wa 2022, nchi zote mbili zilitia saini hati mpya ya makubaliano kuhusu “kubadilishana taarifa za kiufundi na ushirikiano katika usalama wa nyuklia.”
- Mwaka wa 2023, Jarida la Wall Street liliripoti kuwa Marekani ilikuwa ikifikiria kuanzisha shughuli ya urutubishaji wa urani inayoendeshwa na Washington ndani ya ardhi ya Saudi Arabia.
- Mnamo Novemba 2025, nchi hizo mbili zilitia saini tamko la pamoja ambalo, kulingana na utawala wa Donald Trump, “linaweka msingi wa kisheria kwa ushirikiano wa nishati ya nyuklia wenye thamani ya mabilioni ya dola.”
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi