
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty ametoa wito kwa utawala wa kizayuni wa Israel kujiondoa katika Ukanda wa Ghaza na kufungua tena kivuko cha mpakani cha Rafah kuliingana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa Oktoba mwaka jana.
Abdelatty alitoa wito huo Jumapili mjini Cairo katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Christopher Landau, ambapo wawili hao walijadili uhusiano wa pande mbili na matukio ya kikanda.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema, wanadiplomasia hao walibadili mawazo kuhusu njia za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Misri na Marekani, na njia za kuendeleza uhusiano wa pande mbili katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.
Majadiliano yao yalihusu pia yanayojiri katika eneo la Ghaza, Sudan, eneo la Pembe ya Afrika, na usalama wa maji wa Misri.
Abdelatty alisisitizia umuhimu wa kutekelezwa majukumu ya awamu ya pili ya mpango wa Trump kuhusu Ghaza, kuungwa mkono kamati ya kitaifa iliyopewa jukumu la kuendesha eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro, na kupelekwa haraka kikosi cha kimataifa cha kurejesha uthabiti ili kufuatilia usitishaji mapigano.
Aidha, alitilia mkazo udharura wa kufunguliwa tena kivuko cha Rafah kilichopo katika mpaka wa pamoja wa Ghaza na Misri katika pande zote mbili na kufanikishwa uondokaji wa jeshi la Israel huko Ghaza ili kuandaa mazingira ya kutekelezwa mapema ujenzi upya wa eneo hilo.
Siku ya Jumapili, Redio ya Jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel iliripoti kwamba Washington ilikuwa imefikia makubaliano na waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu kuhusu kufunguliwa tena kivuko cha Rafah, ambayo ni njia muhimu ya kupitishia misaada kuelekea Ghaza.
Tovuti ya habari ya Israel ya Walla imedai kuwa, kivuko hicho kinatarajiwa kufunguliwa baadaye wiki hii…/