Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kwamba nidhamu ya dunia inazidi kumomonyoka huku utawala wa sheria ukifutwa, na nafasi yake kuchukuliwa na kile alichokiita “sheria ya msituni.”

Guterres ametoa indhari hiyo alipohutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika wenye makao makuu ya umoja huo kwa anuani ya: “Kuthibitisha upya hali ya sheria ya kimataifa: mikakati ya kuhuisha amani, haki na ushirikiano wa kimataifa,” ukiangazia njia za kurekebisha ukiukaji wa sheria unaoongezeka na unaohatarisha uthabiti wa dunia.

Amesema hadhi ya sheria za kimataifa inashushwa chini katika migogoro na maeneo kadhaa duniani.

“Kutoka Ghaza hadi Ukraine, kutoka Sahel hadi Myanmar na Venezuela, hali ya sheria leo inachukuliwa kama menyu ya kula kwa chaguo,” amesema Guterres, huku akionya kwamba utekelezaji wa kuchagua ni chanzo cha kutokuwepo usawa na kudhoofisha uthabiti.

“Duniani kote, utawala wa sheria unabadilishwa na sheria ya msituni,” ameeleza Katibu Mkuu wa UN na kuongezea kwa kusema: “tunaona ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na kupuuzwa kwa wazi Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

Guterres ameendelea kubainisha kwa kusema: “ukiukaji huu unaunda mifano hatari, ukihimiza nchi nyingine kuchukua hatua kwa maslahi yao wenyewe”.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemalizia hotuba yake kwa kusema: “kupitia utendaji wangu na juhudi zisizo na kikomo za wajumbe na wadau wa Umoja wa Mataifa, nipo tayari kusaidia Baraza hili kuendeleza hali ya sheria na kujenga dunia salama na thabiti kwa wote”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *