Kijana wa kike wa kiisraeli aitwaye Noya Zion ameshtuka baada ya kuona picha yake inaonyeshwa kwenye televisheni ya taifa ya Israel kama mmoja wa watu waliouawa katika maandamano nchini Iran, mkasa ambao umezidi kudhihirisha jinsi utawala huo wa kizayuni unavyosambaza habari feki na za uwongo kuhusu machafuko ya hivi karibuni nchini Iran na namna serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ilivyokabiliana nayo.

Zion, ambaye hajawahi kutia mguu wake katika ardhi ya Iran, alikuwa nyumbani kwao jana Jumatatu alipotazama Chaneli 12 ya habari ya Israel na kuona picha yake ikionyeshwa chini ya kichwa cha habari kilichodai “Wayahudi Wanne Wauawa Katika Maandamano nchini Iran.”

Ripoti hiyo ilimtambulisha Zion kiuwongo kama Sanaz Javaherian, mtu ambaye chaneli hiyo imedai alikuwa mwandamanaji aliyekamatwa na kupigwa hadi kufa na vikosi vya usalama vya Iran.

“Sikuwahi katu kufikiria kama lingenitokea hili maishani mwangu… Niko nyumbani kwetu!” alisema Zion katika video aliyoisambaza haraka kwenye mitandao ya kijamii, akijirekodi pamoja na matangazo ya upotoshaji yaliyorushwa hewani na televisheni ya utawala wa kizayuni. “Niko hapa, niko hai, nimekaa nyumbani, na baada ya nusu saa nitakwenda kufanya mazoezi. Sijawahi kwenda Iran maishani mwangu”, amesisitizia msichana huyo.

Kipande hicho cha video kimezidi kudhihirisha upuuzi wa habari bandia na za upotoshaji zinazosambazwa na utawala wa kizayuni wa Israel kuhusu hali ya mambo nchini Iran.

Wakati huo huo, kisa hicho cha Zion kimeibua mijadala kwenye majukwaa ya kijamii kama X, ambapo watumiaji wamelielezea hilo kama mfano mmojawapo wa “propaganda za Israel”. Andiko moja limesema: “propaganda ya Israel ina ufanisi mkubwa kiasi kufika hadi ya hata kuwaua walowezi wake kwenye TV”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *