Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel ametoa wito kwa nchi kote ulimwenguni kusitisha uhusiano wao na utawala wa Israel na kuweka vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala huo.

Francesca Albanese sambamba na kukosoa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na utawala wa Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, amesisitiza kwamba nchi za dunia zinapaswa kusimamisha uhusiano wao na utawala huo hadi Tel Aviv itakapofuata sheria za kimataifa.

Albanese amsema kwamba utawala wa Israel hauna haki ya kuzuia shughuli za mashirika ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina. Kauli hizi zilitolewa baada ya utawala wa Israel kubomoa makao makuu ya Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) huko Baytul-Muuqaddas Mashariki iliyokaliwa kwa mabavu, hatua ambayo haijawahi kutokea na ambayo, kulingana na msemaji wa UNRWA, imeharibu ofisi na vituo vya mafunzo vya shirika hilo la kimataifa.

Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel amesisitiza kwamba, vitendo vya utawala wa Israel vinaonyesha kupuuza kabisa sheria za kimataifa na jaribio la kuharibu misheni za kibinadamu za Umoja wa Mataifa, na kwamba umewadia wakati kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kusimamisha uanachama wa Israel katika jumuuiya hiyo na kuweka vikwazo vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kufanya biashara ya silaha na utawala huo.

Disemba mwaka jana (2025) Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) lilipasisha  sheria ya kukata umeme na usambazaji wa maji kwa majengo ya UNRWA yaliyoko Baitul Muqaddas Mashariki.

Huko nyuma pia, Israel ilichukua hatua kama hizo za uadui dhidi ya UNRWA. Mnamo mwaka 2024, Knesset ilipasisha sheria ya kupiga marufuku shughuli za shirika hilo la Umoja wa Mataifa huko Israel, ikidai kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walihusika katika matukio ya Oktoba 7, 2023, madai ambayo shirika hilo limeyakanusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *