
Dar es Salaam. Shule ya Sekondari Feza Boys imejivunia uwekezaji mkubwa ulioufanya katika kuwaandaa wanafunzi wake kielimu baada ya kufaulisha wanafunzi wote kwa kupata daraja la kwanza katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Mwalimu wa Taaluma, Said Hassan, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana Januari 31, 2025 katika shule hiyo iliyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam, baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani huo.
Hassan amesema matokeo hayo hayakupatikana kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu uliofanywa na shule hiyo, sambamba na uwepo wa mazingira bora ya kujifunzia yanayomjenga mwanafunzi kuwa bora kitaaluma na kimaisha.
Ameeleza kuwa shule hiyo ina walimu wa kutosha, hali inayowezesha uwiano mzuri kati ya mwalimu na mwanafunzi, ambapo kila mwalimu hufundisha wastani wa wanafunzi 10.
“Feza Schools haitoi mwanafunzi bora katika kupata alama A pekee, bali humjenga mwanafunzi kuwa bora katika nyanja zote. Sisi hatujengi mwanafunzi apate A tu, bali pia awe na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kulingana na wakati uliopo,” amesema Hassan.
Ameongeza kuwa shule imeweka programu mbalimbali za kitaaluma zinazolenga kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani yote ya ndani ya shule pamoja na mitihani ya kitaifa.
“Tumeweza kuwapangia programu zinazowawezesha kufanya vizuri katika mitihani yao yote ya shule na hata mtihani wa Taifa,” amesema.
Hata hivyo, Hassan amesema licha ya kufaulisha darasa zima kwa wastani wa daraja la A, shule hiyo bado haijaridhika kikamilifu na matokeo hayo kwa kuwa matarajio yao yalikuwa makubwa zaidi.
Kwa upande wake, mmoja wa wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja la A katika masomo yote na kuwa kinara wa shule hiyo, Criss Mwingila, amewashukuru walimu na wazazi kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kujifunzia yaliyowawezesha kupata muda wa kutosha wa kujisomea.
Mwingila amesema siri ya mafanikio yao ni mpango wa kufanya mitihani ya majaribio mara kwa mara, ndani na nje ya shule, hali iliyowawezesha kuzoea mitihani na kuichukulia kama jambo la kawaida.