WAKATI Dodoma Jiji ikishuka uwanjani leo kuikabili Mbeya City, kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah amesema hawaingii kazini wakimtegemea mchezaji mmoja, Wiliam Edgar bali wapo wengine wenye uwezo wa kumaliza mchezo.

Kwa hivi karibuni Edgar amekuwa na kiwango bora akifunga mabao katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Yanga walipolala 3-1 na juzi wakati wakiiangusha JKT Tanzania kwa bao 1-0 na kukaa katika nafasi ya tisa kwa pointi 13.

Timu hiyo ambayo haikuwa na mwanzo mzuri, kwa sasa imeonekana kuwa imara, ambapo katika mechi tano zilizopita imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza mmoja dhidi ya Yanga.

Josiah amesema wakati wakiikabili Mbeya City, watakuwa makini kutokana na hali waliyonayo wapinzani, lakini matokeo mazuri waliyonayo Dodoma Jiji yanawapa nguvu na matumaini ya kufanya kweli.

Amesema Edgar amekuwa bora, lakini si mchezaji ambaye wanamtegemea kwa kila kitu badala yake wanategemea matokeo ya timu kwa ujumla na kwamba wapo wachezaji wenye kuweza kuamua iwapo nyota huyo atabanwa.

“Wakimbana Edgar, kuna Beno Ngasa, George Makang’a, Dickson Ambundo, Idd Kipagwile, Elias Maguli, Yassin Mgaza na Anuari Jabir, wote hawa wanaweza kufanya kazi eneo la mbele,” amesema Josiah.

Kocha huyo wa zamani wa Biashara United, Tunduru Korosho na Tanzania Prisons, ameongeza kuwa mkakati wao ni kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo akieleza kuwa anaendelea kuisuka zaidi timu.

Kwa upande wake winga Beno Ngassa amesema baada ya kusota mechi za mwanzoni bila kupata matokeo mazuri, kwa sasa ari na morali imeamka upya kutokana na kile walichovuna katika mechi za hivi karibuni.

Amesema kiwango alichonacho kwa sasa si juhudi zake binafsi bali ushirikiano na wenzake kikosini na maelekezo ya benchi la ufundi akieleza kuwa matarajio yao ni kuona wanaendelea kufanya vizuri.

“Tunacheza kama timu na hatukuwa na mwanzo mzuri, lakini tunashukuru kwa sasa tumebadilika na tunahitaji kulinda tulichonacho, si juhudi binafsi bali ni maelekezo ya kocha na ushirikiano kikosini,” amesema Ngasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *