Nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameanzisha mgomo wa kuichezea Al Nassr huku ikiripotiwa kuwa kile kilichopelekea agome kisipofanyiwa kazi, ataondoka katika klabu hiyo na Ligi ya Saudi Arabia kiujumla.
Sababu ya mchezaji huyo anayelipwa kiasi cha Pauni 488,000 (Sh1.7 bilioni) kwa siku kugoma kucheza na kufikiria kuondoka Al Nassr imetajwa kuwa ni hisia zake kwamba klabu yake haitendewi haki na inanyanyaswa na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF).
PIF ndio inasimamia asilimia 75 ya hisa kwenye klabu nne kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambazo ni Al Ahli, Al Nassr, Al Hilal na Al Ittihad.
Mshambuliaji wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo. Picha na Mtandao
Inasemekana Ronaldo anaamini kwamba kuna upendeleo ambao umekuwa ukifanywa na PIF kwa timu za Al Ittihad, Al Hilal na Al Ahli huku Al Nassr ikikandamizwa.
Suala hilo limeibuka muda mfupi baada ya Al Hilal kukamilisha uhamisho wa Karim Benzema kutoka Al Ittihad huku timu hiyo ikiwa pointi moja nyuma ya Al Nassr inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Saudi Arabia, jambo ambalo Ronaldo anaamini limefanyika makusudi ili kuiongezea nguvu Al Hilal na kuidhohofisha Al Nassr.
Inaripotiwa Ronaldo anadai kwamba Kocha wa Al Nassr, Jorge Jesus hajapata fungu la kutosha kutoka mfuko huo kulinganisha na wapinzani wao ingawa uhamisho wa Benzema unatajwa kufadhiliwa na wawekezaji wa nje na sio PIF.
Mshambuliaji wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo. Picha na Mtandao
Mshambuliaji huyo alianza mgomo wake Jumatatu ambapo hakuonekana uwanjani katika ushindi wa bao 1-0 wa Al Nassr dhidi ya Al Riyadh.
Na vyanzo vya karibu vya mshambuliaji huyo vinafichua kuwa hatoishia kugoma tu bali anajiandaa kulazimisha kuondoka klabuni hapo na kwenda katika Ligi ya Marekani au nyingine kubwa Ulaya.
Huku mkataba wake ukiwa umebakiza muda wa miezi 18, kipo kipengele cha kuuvunja kwa Pauni 43 milioni (Sh152 bilioni) ambacho kinatajwa kinaweza kutumiwa na Ronaldo kutimiza mpango wake huo.