Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi limetangaza kuwa, limekaribisha kwa mikono miwili mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani yaliyofanyika Muscat Oman.

Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uuajemi (GCC) Jassim Mohammed Al-Badawi amesema kuwa, baraza hilo limekaribisha na kufurahishwa na mazungumzo ya Ijumaa kati ya Marekani na Iran nchini Oman.

Aliongeza: “Tunaithamini nchi rafiki na ya kindugu ya Oman kwa kuandaa mazungumzo haya. Hatua hii inaonyesha jukumu la kujenga la Oman katika kuunga mkono mazungumzo ya kikanda na kimataifa.”

Al-Badawi amesema kuwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba linatumai kwamba mazungumzo haya yatatoa matokeo chanya katika kuimarisha amani, usalama, na utulivu katika eneo la Asia Magharibi.

Aidha Katibu Mkuuu wa GCC amesisitiza: “Nchi wanachama wa baraza hilo zinasisitiza kulindwa utulivu na usalama wa eneo hili na ustawi wa watu wake.”

Wawakilishi wa Iran na Marekani jana walifanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Muscat, Oman kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa Iran na kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja na Marekani huko Muscat Oman yamekuwa na mwanzo mzuri, huku hatua za baadaye zikitegemea mashauriano katika miji mikuu.

Oman imekuwa na jukumu kubwa kama mpatanishi kati ya nchi za kikanda katika miaka ya hivi karibuni, na mazungumzo ya jana yanaonekana kama mwendelezo wa mpango wa kidiplomasia wa nchi hiyo wa kupunguza mivutano  na mizozo katika eneo hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *