
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetangaza katika taarifa yake kwamba, hospitali zilizobaki zinazofanya kazi katika Ukanda huo, ambazo zinajitahidi kuendelea kutoa huduma za kimatibabu, zimekuwa vituo vya kusubiri maelfu ya wagonjwa na majeruhi ambao wanakabiliwa na hatima isiyojulikana.
Taarifa hiyo inasisitiza kwamba, athari za mauaji ya kimbari ya kimatibabu zimeathiri vibaya huduma za afya, na kufanya kuendelea kutoa huduma za afya za kila siku kuwa muujiza na changamoto kubwa kwa ajili ya ukarabati mpya wa huduma maalumu.
Takwimu zinaonyesha kwamba akiba ya dawa na vifaa tiba imefikia sifuri katika visa vingi: 46% ya orodha ya dawa muhimu, 66% ya vifaa tiba, na 84% ya vifaa vya maabara na benki za damu havipo. Hata dawa rahisi zaidi za kutuliza maumivu sasa zimekuwa bidhaa ya kifahari kwa watu wanaokabiliwa na kifo wakati wowote.
Wizara ya Afya ya Gaza iliongeza kuwa huduma zinazohusiana na saratani, magonjwa ya damu, upasuaji, huduma ya wagonjwa mahututi na huduma za msingi zimeathiriwa zaidi, na kiasi kidogo cha dawa zinazoagizwa hospitalini hakiwezi kukidhi mahitaji halisi ya kuendelea na huduma za matibabu.
Wizara ya Afya ya Gaza inasema kuwa uhaba huo umelemaza uwezo wa eneo hilo wa kutoa huduma za dharura za matibabu na kuokoa maisha ya wagonjwa kufuatia kuendelea mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza.
Licha ya kusitishwa mapigano huko Gaza, lakini bado mateso ya njaa na ukosefu wa usalama na utulivu wa nafsi yanaendelea kuzisumbua familia za Wapalestina. Foleni ndefu za watu wenye njaa wanaosubiri kupata angalau mlo mmoja kwa siku zinaendelea kuonekana katika pembe mbalimbali za ukanda huo huku jeshi katili la Israeli likiendeleza mashambulizi ya mara kwa mara na kuzuia kuwafikia misaada wananchi hao wasio na ulinzi.