Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, ameridhishwa na maandalizi ya ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo, lililopo Ilala, Jijini Dar es Salaam.
Profesa Shemdoe ameyasema hayo leo, Februari 7, 2026, alipotembelea soko hilo kujiridhisha na maandalizi ya hafla itakayofanyika kesho, kesho ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, atazindua rasmi soko hilo.
Waziri huyo amesema uwekezaji wa Sh28 bilioni uliofanyika katika soko hilo baada ya kuungua mwaka 2021, umetoa soko jipya lenye ghorofa sita, na kuongeza thamani ya biashara katika eneo hilo.
“Namshukuru Rais kwa hatua hii kubwa ya kuwekeza katika soko hili. Hii ni hatua ya kihistoria ambayo tunapaswa kujivunia,” amesema Profesa Shemdoe.
Soko Kuu la Kariakoo liliungua Julai 10, 2021 na Rais Samia alipotembelea eneo hilo baada ya kadhia hiyo, aliahidi kuliboresha.
Profesa Shemdoe amewataka wananchi na wafanyabiashara wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika hafla ya ufunguzi huku akiwapongeza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, uongozi wa Jiji na wa Shirika la Masoko la Kariakoo kwa kushirikiana na kuhakikisha maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha juu.
Ziara ya kiongozi huyo katika soko hilo imeambatana na Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu, Sospeter Mtwale, Katibu Tawala, Abdul Mhinte na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.
Wengine ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabehe, pamoja na viongozi wengine wa wizara.