
KIUNGO mshambuliaji wa Mashujaa FC, Sele Bwenzi amesema licha ya kutofunga bao lolote hadi sasa, bado anajiamini kwa uwezo uwanjani, huku akieleza ugumu na vita ya namba uliopo kikosini.
Bwenzi alikuwa na kiwango bora katika msimu uliopita wakati akikipiga Ken Gold iliyoshuka daraja, ambapo zaidi anakumbukwa kwa bao la umbali alilomtungua kipa wa Yanga, Djigui Diara kwenye mechi iliyoisha kwa Ken Gold kufa mabao 6-1.
Kwa sasa nyota huyo anakipiga kwa Mashujaa, ambapo katika mechi 13 walizocheza hajafunga bao lolote huku akihusika kwenye asisti mbili za mabao na kuifanya timu hiyo kuwa nafasi ya nane kwa pointi 14.
Bwenzi aliliambia Mwanaspoti, kilichomkwamisha kwa sasa katika kikosi hicho ni kukosa namba katika mechi za mwanzo, akieleza kuwa kadri kocha anavyomuamini anaamini atarejesha kasi yake ileile.
Amesema kiu ya wachezaji ni kuipambania timu kupata matokeo mazuri na kwamba kilichowaangusha kwa mechi za karibuni ni kukosa bahati ya kupata ushindi kama ilivyokuwa awali, akitoa matumaini kurejea upya.
“Ushindani wa namba kikosini ni mkali tofauti na nilivyokuwa msimu uliopita, nilikosa namba huko nyuma lakini kwa sasa naamini nitarudi na kasi yangu ni ileile, malengo ni kuona timu inafanya vizuri,” amesema Bwenzi.
Alioongeza baada ya kupitia matokeo yasiyoridhisha katika mechi zilizopita, bado wanayo nafasi ya kujisahihisha kuhakikisha mecji zinazofuata wanaweza kupata ushindi na kujiweka nafasi nzuri.
Alikiri ugumu wa ligi akieleza kuwa upinzani wanaokutana nao kwa timu Ligi kuu unawapa nguvu ya kupambana kuhakikisha wanaondokana na uhaba wa pointi tatu.
“Mashabiki wasikate tamaa kwakuwa tunajua deni letu kwao, bado tunayo nafasi ya kupambana na kubadili matokeo tuliyonayo.”
“Hatujakata tamaa na matarajio yetu ni kufanya vizuri,” amesema staa huyo.