
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kwamba taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, ambayo imerekodi ukatili unaofanywa na utawala vamizi wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina katika vituo na mahabusi zake, inathibitisha zaidi ukiukaji wa sheria za kimataifa ambao haujawahi kutokea unaofanywa na utawala huo.
Hamas imesema kwamba nyaraka za taarifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu aina mbalimbali za mateso ya kimfumo ya Israel na mbinu za kulazimisha, kurubuni na kadhalika wanayofanyiwa mahabusu wa Kipalestina “zinaonyesha vitendo visivyo vya kibinadamu na asili ya uhalifu ya utawala vamizi wa Israel.”
Harakati hiyo imeitaka jamii ya kimataifa, taasisi za Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutumia hati hiyo kwa ajili ya kuchukua hatua za vitendo, ikiwa ni pamoja na kufungua uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu uhalifu wa mateso na unyang’anyi wa kimfumo, kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na uhalifu huo na kuiweka vikwazo Israel ili kuilazimisha kukomesha uhalifu wake na kuwaachilia huru mahabusu wote wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza yake.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imefichua ushuhuda wa kutisha uliotolewa na mateka wa Kipalestina walioachiliwa hivi karibuni, ukizungumzia ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa ndani ya magereza ya Israel, unaofikia kiwango cha uhalifu wa kivita na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba ushuhuda huo unahitaji uchunguzi huru wa kimataifa, ukionya kwamba kutochukuliwa hatua za kuwaadhibu wahusika kunachochea kurudiwa kwa uhalifu kama huo dhidi ya raia wa Palestina.