
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbollah ya Lebanon amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiunga mkono Palestina na watu wanaokandamizwa duniani.
Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika barua kwa Ali Akbar Velayati mshauri wa Kiongozi Mkuu kuhusu masuala ya kimataifa.
Katika barua yake hiyo Katibu Mkuu wa Hizbollah ya Lebanon amezungumzia jukumu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono muqawama na watu wa Palestina, na kusisitiza kwamba katika vita vya hivi karibuni, licha ya kuuawa shahidi kwa makamanda wake na hasara kubwa, Hizbullah iliweza kuzuia uchokozi wa adui.
Sheikh Naim Qassem ameelezea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kama “baraka kubwa ya kimungu,” akiongeza: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefufua dini mkabala wa Mashariki na Magharibi na imekuwa daima msaidizi wa Palestina na wanyonge wa dunia.”
Katibu Mkuu wa Hizbollah pia amezungumzia kusimama kidete Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya vita na vikwazo katika kipindi cha miaka 47 iliyopita, ikiwa ni pamoja na vita vya kutwishwa vya utawala wa Baath wa Iraq na vita vya siku 12 vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kubainisha kwamba, muqawama na kusimama kidete huku ni ishara ya uhalisia wa Mapinduzi ya Kiislamu na ustahiki wa taifa la Iran, na akasifu kujitolea kwa Walinzi wa Mapinduzi na vikosi vya kijeshi na usalama vya Iran.