IRINGA: Wanafunzi wa Shule ya Msingi Jamhuri, iliyopo Kijiji cha Ilongo, Kata ya Ilongo wilayani Mbarali mkoani Mbeya, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama shuleni baada ya kukamilika kwa mradi wa kisima kirefu uliotekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji.
Mradi huo umetokana na utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Mbinu za Asili za Kijamii za Usimamizi wa Vyanzo vya Maji na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (NBS–USANGU), unaofadhiliwa na Serikali ya Japani kupitia Benki ya Dunia.
Kabla ya utekelezaji wa mradi huo, wanafunzi walilazimika kutembea zaidi ya kilometa tatu kutafuta maji, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa masomo, uchovu na wakati mwingine kukosa vipindi vya darasani.
Kupitia mradi huo, kisima kirefu kimechimbwa na maji kusambazwa ndani ya shule pamoja na kwa wananchi wanaoizunguka, hatua inayotarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuimarisha usalama wa watoto.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jenifer Sanga, amesema upatikanaji wa maji ndani ya shule ni mkombozi kwa wanafunzi na walimu.

“Hii ni faraja kubwa kwetu. Sasa wanafunzi hawatapoteza muda kutafuta maji na wataweza kujikita zaidi katika masomo yao,” amesema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ilongo, Benjamini Mwakalonge, amesema mradi huo umemaliza kero ya muda mrefu ya maji katika eneo hilo, akieleza kuwa si wanafunzi pekee watakaonufaika bali pia wananchi wa jirani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, amesema mradi wa NBS–USANGU unalenga si tu kusambaza maji bali pia kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili viwe endelevu.
“Tunataka miradi hii iwe chachu ya maendeleo ya kweli, kwa kuzingatia usimamizi bora wa rasilimali za maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Msimamizi wa mradi kutoka Benki ya Dunia, Nicholas Soikan, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani kuhakikisha miradi ya maji inaleta matokeo yanayokusudiwa.
Naye Mratibu wa Mradi kutoka Bodi hiyo, David Muginya, amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa jamii tangu hatua za mwanzo umechangia mafanikio ya utekelezaji wake.