RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji kuwa na vyuo vikuu vingi zaidi vitakavyosaidia kuiweka Zanzibar katika ramani ya kimataifa kama kituo muhimu cha utoaji wa elimu na mafunzo ya viwango vya juu katika fani mbalimbali.
Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, tarehe 18 Februari 2026, alipokutana na wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mussa Azan Zungu waliofika Ikulu, Zanzibar kwa mazungumzo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi amesema ameridhishwa na wazo la Bunge la kujenga Chuo cha Mafunzo ya Diplomasia na Huduma za Bunge kinachotarajiwa kujengwa Zanzibar akieleza kuwa mradi huo ni fursa muhimu kwa taifa.
Amesema kuwa uwepo wa chuo hicho utachochea ujio wa wanafunzi, wataalamu na viongozi kutoka mataifa mbalimbali kuja kujifunza Zanzibar jambo litakalosaidia kukuza sekta ya elimu pamoja na kuongeza mapato kupitia huduma za malazi, usafiri na biashara ndogo ndogo zinazohusiana na shughuli za kielimu.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia wajumbe hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo. Ameongeza kuwa Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha wazo hilo linatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo kulifanikisha haraka ili Zanzibar iweze kuanza kunufaika mapema.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu amempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uongozi wake thabiti unaoendelea kuleta mabadiliko ya maendeleo Zanzibar hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, huduma za kijamii na kuimarika kwa uchumi unaokwenda sambamba na mabadiliko ya dunia.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge wako Zanzibar kwa ajili ya mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa Kamati ya Uongozi na Tume ya Utumishi ya Bunge. SOMA: Masauni: Wabunge pingeni upotoshaji muungano