Lisbon, Ureno. Staa wa Benfica, Gianluca Prestianni anayedaiwa kumtolea kauli za kibaguzi nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr amejaribu kufafanua kauli alizodaiwa kuzitoa kwa mchezaji huyo na kusababisha mvutano mkubwa katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne usiku.

Mechi kati ya Benfica na Real Madrid ilisitishwa kwa dakika 10 baada ya Vinicius Jr kumtuhumu mchezaji huyo kumtolea kauli za kibaguzi, muda mfupi baada ya kuifungia Madrid bao la kuongoza mjini Lisbon.

Picha za video zilionyesha Vinicius na Prestianni wakisogeleana karibu, kabla ya Prestianni kuinua jezi yake na kufunika mdomo. Muda mfupi baadaye, Vinicius alimkimbilia mwamuzi Francois Letexier kuripoti tukio la kutolewa maneno ya kibaguzi.

Baadhi ya wachezaji wa Real Madrid, wakijaribu kumtuliza nyota wa Benfica,  Gianluca Prestianni baada ya kuripotiwa kumtolea maneno ya kibaguzi mchezaji wa Madrid, Vinicius Jr. Picha na Mtandao

Vinicius alidai Prestianni alimwita ‘tumbili’, dai lililothibitishwa na mchezaji mwenzake Kylian Mbappe aliyekuwa karibu na tukio hilo.

Baadaye Benfica katika taarifa rasmi ya klabu isiyo ya kawaida iliyotolewa Jumatano, asubuhi, ilidai wachezaji wa Real Madrid hawakuwa karibu vya kutosha kumsikia Prestianni.

Kocha Jose Mourinho naye amesema Vinicius aliwachokoza wachezaji wake kwa namna alivyoenda kushangilia bao.

Kupitia Instagram, Prestianni mwenye umri wa miaka 20 amesema: “Ningependa kufafanua sikumtolea kauli za kibaguzi Vinícius Junior, ambaye kwa bahati mbaya alichokisikia alikielewa vibaya. Sijawahi kuwa mbaguzi kwa mtu yeyote na nasikitika kwa vitisho nilivyopokea kutoka kwa wachezaji wa Real Madrid.”

Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr (akiwa kushoto) katika mgogoro na nyota wa Benfica, Gianluca Prestianni wakati akidai kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao

“Kama wanaendelea kusema nilitoa kauli ya kibaguzi kwa Vinicius Junior, basi kwa nini hakuna hata mmoja wao aliyeonyesha hasira wakati natoa kauli hizo. Kumtuhumu mtu kwa jambo zito kiasi hicho si sahihi, watu wote kunishutumu kwa kufunika mdomo kwa jezi yangu wakati wanajua wachezaji wote hufunika midomo wanapozungumza, msipende kuzusha mambo.”

Hata hivyo, nyota wa Madrid Aurelien Tchouameni aliwaambia waandishi wa habari Prestianni alidai hakutoa tusi la kibaguzi.

UEFA inatarajiwa kuanza uchunguzi kuhusu tukio hilo na msemaji wake amesema: “Ripoti rasmi za mechi zilizochezwa juzi usiku zinapitiwa kwa sasa. Ikiwa kutakuwa na lolote litatangazwa kwenye tovuti ya  UEFA.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *