Helios yatoa vifaa vya mil 30/- kukuza TEHAMA shuleniHelios yatoa vifaa vya mil 30/- kukuza TEHAMA shuleni

NYASA, RUVUMA: Wakati taifa likichukua hatua mbalimbali kukuza uchumi wa kidijiti, Kampuni ya Helios Towers imetoa vifaa vya kisasa vya maabara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye thamani ya Shilingi milioni 30/- kwa shule ya Sekondari ya Tingi iliyopo wilayani Nyasa, Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wake kwa jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maabara hiyo ya kisasa shuleni hapo, Mkurugenzi wa Ugavi wa Helios Towers, Baraka Andrew, alisema vifaa vilivyotolewa ni kompyuta 26, ‘projekta’, vifaa vya matengenezo, ‘whiteboard’, TV janja na miundombinu yote muhimu ya maabara.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Helios Towers ilitekeleza mradi huu kwa kushirikiana na shirika la Camara Education Tanzania ambalo lilisimamia na kutekeleza mradi huo kwa pamoja na uongozi wa shule na mamlaka za elimu za wilaya.

Maabara hiyo inatarajiwa kunufaisha zaidi ya wanafunzi 360 kwa kutoa fursa ya kujifunza TEHAMA kwa vitendo, kuongeza ujuzi wa kiteknolojia na kuwaandaa kwa ajira na kushiriki katika uchumi wa kidigitali.

Aliongeza kuwa mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa Helios Towers Tanzania wa uwekezaji katika jamii, ukiunga mkono jitihada za serikali na wadau wa elimu katika kuboresha ubora wa elimu na kuendeleza maendeleo ya kidigitali miongoni mwa kizazi kipya.

SOMA: Ulipaji kodi kidijiti wapigiwa chapuo

“Helios Towers imeona umuhimu mkubwa wa kushiriki kuandaa vijana kuingia kwenye uchumi wa kidijitali, eneo ambalo Rais Samia pia anaweka mkazo mkubwa kuhakikisha Tanzania inafikia kiwango cha juu kinacholingana na kasi ya maendeleo ya dunia,” alisema Andrew.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Kiufundi na Meneja wa Nchi wa Camara Education Tanzania, Dayani Mbowe, alisema kompyuta zilizotolewa zimewekwa na mifumo mbalimbali ikiwemo mitihani, vitabu, na notisi kwa ajili ya wanafunzi kujisomea.

“Mifumo iliyowekwa shuleni na mafunzo yaliyotolewa kwa wanafunzi na walimu imezingatia mahitaji ya mtaala mpya ulioboreshwa, kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tingi kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Wilaya ya Nyasa alimshukuru Helios Towers kwa kufadhili mradi huu na Camara Education kwa kufanikisha ufungwaji na kuweka maudhui yanayostahiki, hivyo kuwawezesha wanafunzi kupata vitabu na nyenzo za kujisomea kwa urahisi mtandaoni.

“Dunia ya leo inazidi kuendeshwa na matumizi ya TEHAMA katika kila kipengele cha maisha. Hivyo, wanafunzi hawa hawatanufaika tu kielimu bali pia watapata ujuzi unaowawezesha kuanzisha shughuli zao za kipato, ikiwemo biashara za steshenari, baada ya kukamilisha ngazi mbalimbali za elimu,” aliongeza Afisa Elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *